Jan 15, 2023 22:55 UTC
  • Jumatatu, Januari 16, 2023

Leo ni Jumatatu mwezi 23 Mfunguo Tisa Jamadi Thani, mwaka 1444 Hijria, sawa na Januari 16 mwaka 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita yaani tarehe 16 Januari 2001 Milaadia, Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya. Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania. Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi. Tarehe 26 Januari 2001, Joseph Kabila mwana wa Rais Kabila alishika hatamu za uongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Laurent Desire Kabila

 

Miaka 65 iliyopita yaani tarehe 29 Dey 1334 Hijria Shamsia, Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika kipindi cha utawala wa Shah hapa nchini Iran. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini Iran baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Sayyid Mujtaba Navvab Safavi

Tarehe 26 Dey 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alitoroka nchini kwa kisingizio cha kwenda kupata matibabu nje ya nchi, baada ya kushadidi wimbi la harakati za Mapinduzi. Muhammad Reza Pahlavi alichukua kiti cha ufalme mwaka 1320 Hijria Shamsia baada ya serikali ya Uingereza kumpeleka uhamishoni baba yake, Reza Shah, kwa sababu aliiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Siku chache kabla ya tukio hilo, Imam Ruhullah Khomeini ambaye wakati huo alikuwa Ufaransa, alitoa ujumbe mzito akisema kuwa: "Safari ya Shah bila ya kung’oka madarakani haitabadilisha lolote na utawala wa kifalme nchini Iran unapaswa kuangushwa kikamilifu."

Wakati Mfalme Shah wa Iran alipoikimbia nchi mwaka 1978

 

Katika siku kama ya leo miaka 177 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo. Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas. Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.

Mchoro wa vita vya Marekani na Mexico vya mwaka 1846

 

Miaka miaka 66 iliyopita katika siku sawa na ya leo alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki.

Arturo Toscanini