Alkhamisi, 19 Januari, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadithani 1444 Hijria mwafaka na tarehe 19 Januari 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika kwa Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waende kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi. ***
Miaka 618 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, Sheikh Jamaluddin Miqdad Hilli Asadi, fakihi na msomi wa Kiislamu aliaga dunia huko Najaf, moja ya miji ya Iraq. Hakuna taarifa kuhusiana na tarehe yake ya kuzaliwa, lakini lililo bayana ni kwamba, alikuwa mwenyeji wa mji wa Hillah Iraq. Alikuwa mashuhuri baina ya Maulamaa kwa jina la Fadhil Miqdad na alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Muhammad bin Makki. Fadhil Miqdad ameacha turathi na dafina kubwa ya vitabu na miongoni mwa vitabu vyake ni Adab al-Hajj na Ayat al-Ahkam.***
Siku kama hii ya leo miaka 287 iliyopita alizaliwa mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini. ***
Miaka 225 iliyopita inayosadifiana na siku hi ya leo, alizaliwa Auguste Comte mwanafalsafa, mwanahisabati wa Kifaransa na mtaalamu wa falsafa umbile au positivism kwa kimombo. Comte alifikia daraja ya uhadhiri katika hisabati akiwa na umri wa miaka 18 tu. Vitabu mashuhuri vya mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni Auguste Comte and positivism na Early Political Writings. Comte aliaga dunia mwaka 1517. ***
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran wenye imani na umoja walifanya maandamano makubwa kupinga mabaki yaliyosalia ya utawala wa kifalme Shah, yaani serikali ya Shapur Bakhtiyar. Wafanya maandamano hao walitaka serikali hiyo ya kifalme itangazwe kuwa si halali, na pia kung'olewa utawala wa Shah na badala yale kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. Siku hiyo Imam Khomeini MA akiwa mjini Paris alitoa ujumbe wa maandishi kwa wananchi wa Iran akisema kama tunavyonukuu: "Kwa uwezo wake Mola hivi karibuni nitaungana nanyi ili niweze kuwatumikia na kushirikiana bega kwa bega na matabaka yote ya wananchi kuelekea katika njia ya kujitawala na kuwa huru Iran." Mwisho wa kunukuu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, Abdul Rauf Mahmoud al-Mabhuh, mmoja wa makamanda waandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) aliuawa shahidi huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mabhouh aliuawa na makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel walioingia nchini Imarati wakitumia pasipoti bandia. Mabhuh alizaliwa katika familia iliyoshikamana na dini katika kambi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza, Palestina. Shahidi Mahmoud al-Mabhuh ni miongoni mwa waasisi wa Brigedi ya Izzudeen al-Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Baada ya kupita miezi kadhaa, Israel ilitangaza wazi kwamba, ilihusika na jinai ya kumuua Mabhuh. ***
Na siku ya leo tarehe 29 Dei inajulikana nchini Iran kwa anwani ya "Siku ya Gaza". Siku hii ni kumbukumbu ya kumalizika vita vya siku 22 vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza ambapo vita hivyo vilifikia tamati kwa ushindi wa muqawama na mapambano ya Kiislamu huko Gaza. Kutokana na vyombo vya Magharibi kuficha jinai za utawala haramu wa Israel na kwa upande mwingine kutokana na hamasa kubwa iliyooonyeshwa na wananchi madhulumu wa Gaza katika kutetea ardhi zao, siku hii imepewa jina la "Siku ya Kitaifa ya Gaza. ***