Jan 20, 2023 22:53 UTC
  • Jumamosi, 21 Januari, 2022

Leo ni Jumamosi 28 Mfunguo Tisa Jamadithani 1444 Hijria, sawa na 21 Januari 2023 Miladia.

Katika siku kama hii ya leo miaka 854 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatibi, msomi mashuhuri wa Qur'ani aliyekuwa maarufu kwa jina la Imamul Qurra. Abul-Qasim alizaliwa mwaka 538 Hijiria. Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika taaluma ya usomaji wa Qur'ani, alikuwa pia mtaalamu wa elimu ya tajweed, tafsiri ya Qur'an, hadithi, sarufi ya lugha ya Kiarabu na elimu nyinginezo za kipindi hicho. Licha ya kuwa kipofu lakini alisifika kwa kuwa hodari na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani mwake. Msomi huyo wa Kiislamu ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kiitwacho "al Qasidatus Shatwibiyyah" kilichokusanya masuala yanayohusiana na elimu ya tajweed. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 277 iliyopita tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo. Ghuba ya Bengali iko kaskazini mwa Bahari ya Hindi na kusini mwa Asia na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali. ***

 

Siku kama ya leo miaka 230 iliyopita Mfalme Louis XVI wa Ufaransa alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XVI kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XIV akiwemo mkewe Marie-Antoinette pia walinyongwa. ***

Mfalme Louis XVI wa Ufaransa

 

Miaka 142 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alim na fasihi wa Kiirani Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani. Mbali na kubobea katika elimu ya fiq'hi, Tankabani pia alikuwa mtaalamu katika fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake. Muhammad bin Suleiman ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na "Al Fawaidu fii Usuliddin" na " Qisasul-Ulama." Katika kitabu hicho kilichochapishwa mara kadhaa nchini Iran alizungumzia maisha ya maulama wa kabla yake. ***

Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani.

 

Siku kama ya leo miaka 44 liyopita sambamba na kuanza kutetereka nguzo za utawala wa Shah nchini Iran mkabala wa wimbi kubwa la mashinikizo ya wananchi na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu, serikali ililazimika kuwaachia huru wafungwa waliokuwa katika jela za Shah na wananchi Waislamu wa Iran wakawapokea watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa miaka mingi katika jela hizo. Alasiri ya siku hiyo maafisa wa Jeshi la Anga la Iran walifanya maandamano na kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati ya taifa la Kiislamu la Iran. Siku hiyo hiyo pia magazeti ya Iran yaliandika habari iliyokuwa na kichwa kilichokolezwa wino kwamba: "Imam Khomeini Kurejea Iran Siku Kadhaa Zijazo". Habari hiyo ilizusha wimbi la hamasa na furaha kubwa kati ya wananchi wanamapinduzi wa Iran na kila mtu alianza kujitayarisha kwa ajili ya kwenda kumpokea kiongozi wa kihistoria wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini. ***

Imam Ruhuullah Khomeini