Jumapili, 22 Januari, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 29 Mfunguo Tisa Jamadithani 1444 Hijria, sawa na tarehe 22 Januari 2023 Miladia
Siku kama ya leo miaka 462 iliyopita inayosadifiana na tarehe 22 Januari 1561 alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon. Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626.
Miaka 248 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana fani ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836.
Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malkia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64. Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ilikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII.
Miaka 44 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, ikiwa ni katika muendelezo wa wananchi Waislamu wa Iran kuupinga utawala wa Shah na kukabiliana na wanajeshi wa utawala huo, idadi kubwa ya raia waliuawa na kujeruhiwa. Wananchi wa Iran ya Kiislamu wambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa kurejea nchini Imam Khomeini (M.A) walitayarisha mazingira hitajika kwa ajili ya mapokezi makubwa zaidi ya kihisitoria kwa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mnasaba huo, wafanyakazi mbalimbali wakiwemo maulamaa na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wakazi wa mji wa Tehran walikusanyika pamoja ili kuandaa hafla kubwa ya kumpokea Imam. Watu wengi kutoka katika miji na vijiji vya Iran ya Kiislamu walimiminika kwa wingi mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika sherehe za kumkaribisha Imam Khomeini (M.A). Katika upande mwingine, baada ya maandamano makubwa ya wananchi, wanajeshi elfu nne wa jeshi la anga pia waligoma kula wakitaka kuondoka Iran washauri wa kijeshi wa Marekani katika kuwaunga mkono wananchi wanapambano wa Iran.
Na tarehe 22 mwezi Januari mwaka 1979 ; miaka 44 iliyopita mwanamapambano wa Kipalestina Abu Hassan Salameh aliuawa kigaidi na maajenti wa utawala wa Kizayuni. Abu Hassan Salameh ndiye aliyepanga na kuratibu oparesheni ya kuwateka nyara Waisraili 12 katika mashindano ya Olimpiki huko Munich Ujerumani mwaka 1972. Salameh alikuwa Kamanda wa Jeshi la Vita Vitakatifu vya Palestina katika Vita vya Palestina vya mwaka 1948. Oparesheni hiyo ilitekelezwa Septemba 5 mwaka 1972 na kupelekea kuuawa mateka 12 wa Israel, Wapalestina 5, polisi mmoja wa Ujerumani na kutiwa nguvuni Wapalestina 3. Abu Hassan ndiye aliyepanga oparesheni hiyo japokuwa mwenyewe hakushiriki moja kwa moja kwenye oparesheni hiyo. Abu Hassan Salameh aliuliwa kigaidi Januari 22 mwaka 1979 miaka saba baada ya oparesheni ya Munich. Aliuawa katika moja ya mitaa ya Beirut akiwa na wenzake wanne wakati walipotoka nje ya nyumba baada ya kuripukiwa na bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari mkabala wa nyumba yake.