Jumatatu, 23 Januari, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe Mosi ya mwezi wa Rajab 1444 Hijria mwafaka na tarehe 23 Januari 2023 Miladia.
Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab. ***
Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. ***

Miaka 191 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia. Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883. ***
Katika siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia. Aliongoza na kutengeneza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni. Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.***
Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa. ***
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. ***
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Bahman 1357 Hijria Shamsia, baada ya kupatikana uhakika kuhusiana na uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, kuliundwa kamati ya mapokezi ya Imam Khomeini. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50,000 ikiwa na mjumuisho mkubwa wa wawakilishi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam Khomeini, kumlinda, kuweka nidhamu, kulinda usalama na kudhamini mambo ya lazima kwa ajili ya kurejea Imam Khomeini. ***
