Jan 24, 2023 22:58 UTC
  • Jumatano, 25 Januari, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 3 ya mwezi wa Rajab 1444 Hijria ambayo inali9ngana na tarehe 25 Januari 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.***

 

Katika siku kama ya leo miaka 567 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. ****

 

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Ujerumani kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani. ***

Gerhard Henrik Armauer Hansen

 

Tarehe 5 Bahman miaka 44 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji. Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran. Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah. Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu. ***

Miaka 17 iliyopita katika siku  kama ya leo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS