Jan 26, 2023 22:39 UTC
  • Ijumaa, 27 Januari, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Rajab 1444 Hijria mwafaka na tarehe 27 Januari 2023 Miladia.

Tarehe 5 Rajab miaka 1200 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik." ***

 

Miaka 132 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 vikiwemo vya "Tufani" na "Kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967. ***

 

Miaka 90 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ayatullah Muhammad Baqir Hujjati Mazandarani msomi na mwanazuoni mkuubwa wa Kiirani. Alizaliwa 1248 jirani na Babul moja ya miji ya kaskazini mwa Iran. Alikuwa yatima baada ya kuzaliwa hali ya kuwa baba yake ameshafariki dunia. Familia ya Ayatullah Hujjati ilikuwa ya watu walioshikamana na elimu. Muhammad Baqir naye aliafuata njia na mkondo huo huo. Mbali na mchango mkubwa aliokuwa nao katika kueneza maarifa na mafundisho ya dini kwa njia ya kufundisha, mwanazuoni huyu hakuwa nyuma pia katika taaluma ya utunzi na uandishi wa vitabu. ***

Ayatullah Muhammad Baqir Hujjati Mazandarani

 

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964. ***

Vita vya Vietnam