Jan 29, 2023 23:15 UTC
  • Jumatatu, Januari 30, 2023

Leo ni Jumatatu mwezi 8 Rajab 1444 Hijria inayosaidfiana na tarehe 30 Januari 2023, Milaadia.

Siku kama ya leo mwezi 8 Rajab, yaani miaka 411 iliyopita kwa mujibu wa kalenda na Hijria, alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa zama hizo hususan katika elimu za fiqhi na Hadithi. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwake ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Ummah. Mwanazuoni huyo aliaga dunia mwaka 1114 Hijria.

Sheikh Hurr al Aamili

 

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya jeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika kwenye mitaa mbalimbali ya Tehran. Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah. 

Siku za mwisho za utawala wa Shah nchini Iran

 

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani. Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo. Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo. 

Adolph Hitler

 

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali. Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini. Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi. 

Mohandas Karamchand Gandhi