Jan 30, 2023 22:49 UTC
  • Jumanne tarehe 31 Januari 2023

Leo ni Jumanne tarehe 9 Rajab 1444 Hijria sawa na Januari 31 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran. Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. Harakati hiyo ilitokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. Lengo kuu la harakati hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.

Siku kama ya leo miaka 424 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. Baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.

Na siku kama hii ya leo miaka 481 iliyopita aliuawa shahidi Izuddin Sayyid Hussein, mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu wa karne ya 10 Hijria. 

Alizaliwa mwaka wa 906 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil huko Lebanon na kujifunza elimu za wakati huo na kupata nafasi za juu za kielimu.

Watu wenye chuki na husda, ambao hawakuweza kuvumilia utu na shakhsia yake kubwa ya kiroho na kidini katika mji wa Sayda (Sidon) huko Lebanon, walimpa sumu mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu na kumuua katika siku kama hii ya leo.