Jumatano, tarehe Mosi Februari, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 10 Rajab 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Februari 2023.
Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar. *

Katika siku kama hii ya leo miaka 1249 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi Al-Jawad AS alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS. Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

Katika siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.
Tarehe Mosi Februari miaka 65 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri. Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa. Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".
Na katika siku kama ya leo miaka 10 iliyoita, Dakta Hassan Habibi mwanasiasa na mwanasheria wa Kiirani alifariki dunia. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1936. Hassan Habibi alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika taaluma ya sosholojia na sheria katika Chuo Kikuu cha Sorbonne mjini Paris Ufaransa. Hassan Habibi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Miongozo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Juu. Aidha alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 2001 katika kipindi cha Urais wa Akbar Hashemi Rafsanjani na Sayyid Muhammad Khatami.