Jumamosi, Juni 18, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 12 Ramadhani mwaka 1437 Hijria, sawa na Juni 18 mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo yaani tarehe 12 Ramadhani kwa mujibu wa wapokezi wengi wa kalenda ya Hijria Qamaria, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam Masih AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.
XXXXXXXXXXX
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhama Makka na kuelekea Madina, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.
XXXXXXXXXXX
Tarehe 12 Ramadhani miaka 840 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.
XXXXXXXXXXXX
Na Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 nchi ya Misri ilitangazwa kuwa ya Jamhuri na Mfalme Farouq wa Misri na wanawe wakabaidishwa. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948, wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya nchi hiyo ikaanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal Abdun Nassir. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.