Feb 12, 2023 23:01 UTC
  • Jumatatu, Februari 13, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 22 Rajab 1444 Hijria, sawa na Februari 13, mwaka 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo mwaka 1946 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani. Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani. 

Tarehe 13 Februari miaka 765 iliyopita mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi, ulitekwa na Hulagu Khan. Hulagu alimuua mtawala al Muutasimu Billah na kukomesha kabisa utawala wa kizazi cha Bani Abbasi uliotawala maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 37. Katika unyama huo mkubwa, Hulagu Khan alifanya ukatili mkubwa na kuua nusu ya watu wasiokuwa na hatia wa mji wa Baghdad. Hulagu Khan pia alichoma moto nyumba na majengo mengi ya kihistoria ikiwemo maktaba kubwa ya Baghdad na idadi kubwa ya vitabu vyenye thamani kubwa vya maktaba hiyo viliteketezwa au kutumbukizwa katika mto Tigris.

Katika siku kama ya leo miaka 216 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utotoni. Awali alisoma masomo ya msingi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama Sayyid Mahdi Bahrul Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi na vilevile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali. Miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyu mkubwa wa Kiislamu ni kile cha Kashful Ghita.

Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa

Na miaka 35 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani. Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr hapa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake. Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake mjini Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chimbuko la uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa. Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu.

Sheikh Salman Khaqani