Feb 14, 2023 07:51 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 12 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni hikma ya 12.

أَعْجَزُ النَّاسِ مَنْ عَجَزَ عَنِ اکْتِسَابِ الاِْخْوَانِ، وَأَعْجَزُ مِنْهُ مَنْ ضَیَّعَ مَنْ ظَفِرَ بِهِ مِنْهُمْ

Mtu dhaifu kuliko wote ni yule asiyeweza kupata marafiki, na aliye dhaifu kuliko yeye ni yule anayempoteza rafiki aliyempata.

Moja ya masuala muhimu zaidi katika maisha ni kuwa na urafiki na wengine. Kuanzia siku ya kwanza watoto wanapoingia kwenye ulimwengu huu na hasa wakati wanapoingia kwenye hirimu ya kuweza kucheza, huwa moja kwa moja wanaanza kufanya urafiki na wengine ikiwa ni sehemu ya lazima na ya wajibu katika maisha ya kila mtu. Huenda urafiki huo ukawa baina yake na watu wa ndani ya familia, lakini lazima anahitajia urafiki. Marafiki ni sehemu muhimu ya maisha yetu. Wanatupa hisia ya kuwa nasi ni sehemu katika jamii. Hutupa furaha na shangwe, hutusaidia na kutuongoza tunapohitaji. Inafurahisha kujua kwamba matokeo ya utafiti wa kisayansi wa miaka ya hivi karibuni yameonesha kwamba watu walio na marafiki wazuri wanakuwa na afya ya akili na wanaishi muda mrefu zaidi.

 

Taathira za rafiki zinaweza kupita hali tuliyo nayo hivi sasa. Yaani, marafiki wetu wanaweza kuathiri sana pia mustakbali wetu. Ushawishi huu una mambo mawili muhimu. Moja ni kwamba athari za ushawishi huo huweza kuonekana baada ya kupita muda mrefu. Hii ina maana kwamba, rafiki anapokuwa mzuri athari zake njema hubakia kwa muda mrefu katika maisha yatu. Pia rafiki anapokuwa mbaya na muovu, humuongoza mtu kidogo kidogo kwenye shimo la maangamizi, mpaka amtie kwenye hasara kubwa Siku ya Kiyama. Qur'ani Tukufu inaubainisha wazi uhakika huo kwenye aya ya 28 ya Surat al Furqan ambayo inasema: 

یا وَیْلَتى‌ لَیْتَنِی لَمْ أَتَّخِذْ فُلاناً خَلِیلًا

Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!

Naam, mpotovu atakapopelekwa kwenye moto wa Jahannam siku ya Kiyama, atajutia maisha yake na atauma vidole akisema: "Ee Ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki!"

Rafiki mzuri ni aina fulani ya mtaji kwa wanadamu. Mtaji ambao ni muhimu si tu katika kuwasaidia watu wakati wa shida, lakini pia ni fursa ya kupata mtu wa kukutuliza moyo wakati wa dhiki na kufaidika na uzoefu na fikra zao. Waswahili tunasema, akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Naye Imam Ali AS anasema katika kitabu cha Ghurar al-Hikam na Durar al-Kalam: 

مَن لا صَدِیقَ لَهُ لا ذُخرَلَهُ

Mtu ambaye hana marafiki, hana akiba wala mtaji

Mtu dhaifu kuliko wote ni yule asiyeweza kupata rafiki, na aliye dhaifu kuliko yeye ni yule anayempoteza rafiki aliyempata.

 

Hapana shaka kwamba moja ya mali muhimu zaidi ya mtu maishani, ni kuwa na marafiki wazuri na mlioshibana. Kama unavyojua mpenzi msikilizaji, kupata rafiki na mtaji kama huu si kazi nzito na ni jambo rahisi. Baadhi ya wakati kupata mali kunahitaji juhudi nyingi kuliko kupata rafiki. Mtu anapokuwa na tabia njema, adabu, mlahaka mzuri na muamala wa kiuadilifu huwa ni rahisi sana kwake kupata marafiki. Kwa hiyo, Imam Ali AS anasema katika hikma hii ya 12 ya Nahjul Balagha kwamba: Mtu dhaifu kuliko wote ni yule asiyeweza kupata rafiki, na aliye dhaifu kuliko yeye ni yule anayempoteza rafiki aliyempata.

Naam, hapo Imam Ali AS ameongeza kuwa, aliye dhaifu zaidi kuliko wote ni yule anayempoteza rafiki mzuri kwa maadili yake mabaya na kutoheshimu haki za wenzake.

Sababu yake ni kwamba, mara nyingi kunahitajika juhudi za kuweza kupata kitu. lakini ni rahisi sana kukihifadhi kitu hicho. Kwa hivyo mtu anayepoteza marafiki zake kwa tabia zake mbaya na kutojali, ni dhaifu zaidi kuliko hata yule aliyeshindwa kupata marafiki.