Feb 15, 2023 02:24 UTC
  • Jumatano, Februari 15, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 24 Rajab 1444 Hijria, sawa na Februari 15 mwaka 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita, ngome ya Khaybar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Muhammad (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakifanya njama zao huko Khaybar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaybar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaybar.

Mabaki ya Ngome ya Khaybar

Katika siku kama ya leo miaka 1105 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan  ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo  mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya  Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

Siku kama ya leo miaka 459 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na kupelekea kuhukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.

Galileo Galilei

Miaka 241 iliyopita tarehe 15 Februari vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba, vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.

Vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza

Miaka 232 iliyopita katika sikuu kama ya leo alifariki dunia Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf. Akiwa mjini hapo haraka alifikia daraja ya umarjaa sambamba na kuteuliwa kuwa mkuu wa hauzana chuo kikuu cha kidini cha mji huo mtakatifu. Alifanya mabadiliko katika chuo hicho kikongwe. Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’hab ya Kishia. Aidha aliwalea wanafunzi wengi, bila kusahau kazi ya kufafanua vitabu. Maulama kama vile Sheikh Jafar Kashif al-Ghitaa, Mulla Ahmad Naraqi, Muhammad Baqir Shafati, Sayyid Muhammad Jawad Aamili…ni baadhi ya wanafunzi wa Sayyid Bahrul-Ulum. Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na muqawama wa mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.