Feb 15, 2023 23:03 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 16 Februari, 2023

Leo ni siku ya Alkhamisi tarehe 25 Rajab 1444 Hijria, sawa na tarehe 16 Februari 2023.

Siku kama ya leo miaka 1261 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo alipata malezi na elimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Ja'far as-Swadiq (as) kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa baba yake, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuongoza Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, na alikumbana na mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kulingania dini na kupambana na madhalimu. Hatimaye Haroun Rashid alimuua mjukuu huyo wa Mtume (saw) kwa kumpa sumu.

Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha Swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'   ***

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. 

Bendera ya Lithuania

Siku kama leo miaka 77 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya Zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa. 

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Bahman, idadi kadhaa ya viongozi wa utawala wa Kipahlavi walinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya usaliti na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Iran. Licha ya kuwa kwa mtazamo wa wananchi Waislamu wa Iran jinai za viongozi hao wa utawala dhalimu wa Shah zilikuwa wazi na bayana, lakini kwa amri ya Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu kuliundwa Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na kushughulikia kesi za viongozi hao waliokuwa wametiwa mbaroni na vikosi vya wananchi.

Nematollah Nasseri

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1992 Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi