Jumanne, tarehe 21 Februari, 2023
Leo ni Jumanne tarehe 30 Rajab 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Februari 2023.
Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia aliyekuwa raia wa Uholanzi.
Dozy alizama katika taaluma za historia na lugha na kupata shabada ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusoma ytamaduni wa Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu.
Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Uislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania.
Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya Kisiasa na Tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu Kuanzia Mwanzo Hadi Katikati ya Karne ya 19' na 'Tamaduni za Mavazi ya Kiislamu.'
Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Katika siku kama ya leo mia 58 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo.
Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.
Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.
Tarehe 21 Februari miaka 50 iliyopita ndege ya abiria ya shirika la ndege la Libya iliyokuwa ikielekea Misri ilidunguliwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ndege hiyo ya raia ilikuwa njiani kutoka Tripoli, mji mkuu wa Libya, kuelekea Cairo, mji mkuu wa Misri, ilipopoteza njia kutokana na hali mbaya ya hewa na kuonekana kwenye jangwa la Sinai kaskazini mwa Misri.
Wakati huo, eneo la Sinai lilikuwa linakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, na ndege za kijeshi za utawala huo ziliishambulia bila kujali kwamba ndege hiyo ya Libya ilikuwa ya abiria. Abiria 108 kati ya 113 waliokuwemo kwenye ndege hiyo waliuawa.
Uhalifu huu uliamsha hasira ya walimwengu na ulilaaniwa piia na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Na miaka 23 iliyopita kwa mara ya kwanza "Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama" iliadhimishwa. Uamuzi wa kuitangaza siku hii kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ulichukuliwa Novemba 1999 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo mwaka 2008 ulipewa pia jina la 'Mwaka wa Kimataifa wa Lugha". Sisitizo la kulinda na kuimarisha lugha ya mama linatokana na kuwa, takribani nusu ya lugha 6,000 zinazotambulika duniani zimo katika hatari ya kutokomea kutokana na sababu mbalimbali hususan uingiaji na utwishaji wa lugha za kimataifa kwa kutumia mbinu mbalimbali.
