Jumatano, Februari 23, 2023
Leo ni tarehe Mosi Shabaan mwaka 1444 Hijria sawa na Februari 22 mwaka 2023 Milaadia.
Mwezi wa Shaabani unaoanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira. Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake wamewausia mno Waislamu kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Siku kama ya leo miaka 751 iliyopita Ghiathuddin Abu Madhaffar Abdul Karim bin Ahmad anayefahamika kwa lakabu ya Ibn Taus, alifariki dunia huko Kadhimain, moja kati ya miji ya Iraq. Ibn Taus alikuwa faqihi na mwandishi mashuhuri wa karne ya saba Hijria. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kiarabu na kupata elimu kwa wanzuioni wakubwa kama Khajah Nasiruddin Tusi. Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu.

Tarehe Mosi Shaabani miaka 178 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahibul Jawahir. Sahibul Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo. Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na umakini mkubwa.
Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Isfand mwaka 1299 Hijria Shamsia, Uingereza ilitekeleza siasa zake za kikoloni kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran. Njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa na maafisa wa serikali ya Uingereza waliokuwa mjini Tehran wakishirikiana na baadhi ya maafisa usalama wa mji huo. Wafanya mapinduzi waliudhibiti mji mkuu baada ya mapigano ya muda mfupi, na Ahmad Shah Qajar akalazimika kumteua Reza Khan kuwa Kamanda Mkuu wa majeshi. Miaka minne baadaye Reza Khan ambaye alikuwa akiungwa mkono na kusaidiwa sana na Waingereza kutokana na kukandamiza harakati za ukombozi za wananchi alifanywa mfalme wa Iran hadi mwaka 1320 Hijria Shamsia, ambapo aliondolewa madarakati na Waingereza wenyewe na kupelekwa uhamishoni baada ya kuegemea upande wa Ujerumani katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Siku kama hii ya leo miaka 65 iliyopita aliaga dunia Abul Kalaam Ahmad Azad, aalim, khatibu hodari na mwanasiasa wa India akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalaam Azad alianzisha harakati za kisiasa dhidi ya ukoloni wa Uingereza na kwa lengo la kuwaamsha Waislamu wa India akiwa na umri wa miaka 17. Mwanasiasa huyo aliwekwa gerezani mara kadhaa kutokana na kuchapisha makala na kutoa hotuba zenye kufichua njama za wakoloni wa Kiingereza.
Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo oparesheni ya kijeshi ya "Khaybar" ilianza wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Oparesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji jasiri wa Iran.
Oparesheni hiyo ambayo ilianza kutekelezwa katika eneo la Hurul Huwaizah huko kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji wa Kiirani walivuka maji na vinasamasi na kukiteka nyara kisiwa chenye utajiri wa mafuta cha Majnuun karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq.
Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita miripuko mikubwa ya mabomu ilitokea katika haram mbili tukufu za Maimamu Hadi na Hassan al Askari (as) huko katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq na kusababisha hasara kubwa katika eneo hilo tukufu la Waislamu.
Uharibifu mkubwa uliosababishwa na miripuko hiyo katika haram hizo tukufu uliwakasirisha Waislamu duniani na hasa wa wafuasi wa madhehebu ya Shia. Maimamu hao wawili ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw).