Feb 25, 2023 04:55 UTC
  • Ijumaa tarehe 24 Februari 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Shaaban 1444 Hijria sawa na tarehe 24 Februari 2023.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu. 

Katika siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka. Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka. Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayah hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu. Aidha akiwa mjini Makka Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo. Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa. 

Miaka 498 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Luis Vaz de Camoens, malenga mkubwa wa Kireno na mmoja wa wanafasihi wakubwa wa Ulaya huko Lisbon mji mkuu wa Ureno. Mbali na kuwa mshairi, De Camoens alikuwa mpiganaji jasiri. Moja ya kazi muhimu za utunzi za Luis Vaz de Camoens ni ile aliyoipa jina la" The Lusiads." 

Luis Vaz de Camoens

Miaka 175 iliyopita katika siku kama ya leo utawala wa muda au duru ya pili ya mfumo wa jamhuri ulianza huko Ufaransa baada ya wananchi kufanya mapambano ya ukombozi na kumuondoa madarakani Luis Phillipe Mfalme mbeberu wa nchi hiyo. Utawala wa aina hiyo unajulikana pia katika historia ya Ufaransa kwa jina la "Utawala wa Waandishi wa Habari". Hii ni kwa sababu waandishi habari 11 waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri chini ya uongozi wa Alphonse de Lamartine malenga na mwandishi wa Kifaransa, ndio waliokuwa wakisimamia utawala huo.   

Luis Phillipe

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alizaliwa Ayatullah Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya kati alielekea Najaf, Iraq na kupata elimu kwa maulama wakubwa wa zama. Alifikia daraja ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 26 na baada ya kurejea Isfahani alijikita katika shughuli ya kufundisha sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake wavue vazi la staha la hijabu, Ayatullah Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran. 

Ayatullah Hussein Khadimi

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita sawa na tarehe 24 Februari 1949 wawakilishi wa Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel walisaini mkataba wa kusitisha mapigano kati ya pande mbili hizo huko katika kisiwa cha Rhodes kilichoko katika bahari ya Aegean. Ni vyema kutaja hapa kuwa baada ya kuundwa serikali ya Kizayuni mwaka 1948 huko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Misri ilishirikiana bega kwa bega na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kupigana vita dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo wanajeshi wa utawala huo walifanikiwa kuingia katika ardhi ya Misri na Lebanon baada ya kuishambulia safu ya vikosi vya mapambano vya Waarabu ambavyo vilikuwa na zana chache za kisasa za kivita na hivyo kutoa pigo kwa vikosi vya nchi za Kiarabu.