Feb 28, 2023 22:47 UTC
  • Jumatano, tarehe Mosi Machi, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 8 Rajab 1444 Hijria sawa na tarehe Mosi Machi mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 882 iliyopita alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa Hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo.

Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza pia elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya awali alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz.

Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau na kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.

Katika siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, ufalme wa siku mia moja wa Napoléon Bonaparte ulianza nchini Ufaransa baada ya Bonaparte kutoroka sehemu aliyokuwa amebaidishwa katika kisiwa cha Elba.

Tarehe 27 mwezi Februari mwaka huohuo akiwa pamoja na wanajeshi elfu moja Napoleon Bonaparte alifanikiwa kutoroka katika kisiwa cha Elba ambako alikaa akiwa uhamishoni kwa kipindi cha miezi kumi na kurejea Ufaransa na utawala wa kifalme ukaanza nchini humo.

Napoléon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita yaani tarehe 1 Machi mwaka 1892 Miladia, alizaliwa mjini Tokyo mwandishi na mtaalamu mkubwa wa Japan anayejulikana kwa jina la "Rhunosuke Akutagawa".

Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu na miongoni mwake ni vitabu vya "Binti wa Buibui" na "Tushi Gun."

Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1927.

Rhunosuke Akutagawa

Miaka 125 iliyopita katika siku kama leo, kisiwa cha Puerto Rico kilichoko katika ya Bahari ya Atlantic kaskazini mwa Amerika ya Kusini, kilikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Marekani baada ya kumalizika vita vya kikoloni vya Uhispania na Marekani.

Baada ya Marekani kukitwaa kwa nguvu kisiwa hicho ilikifanya ghala kubwa la silaha, kiasi kwamba Marekani iliasisi kambi 13 za kijeshi kisiwani humo.

Kisiwa hicho ambacho mara kwa mara hukumbwa na ukosefu wa amani, miongoni mwa nchi zinazozungumza lugha ya Kihispania katika bara la America. 

Kisiwa cha Puerto Rico

Tarehe 10 Esfand miaka 44 iliyopita hayati Imam Ruhullah Khomeini kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika mji wa kidini wa Qum baada ya kuwa uhamishoni nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 15.

Imam alipelekwa uhamishoni na utawala wa Shah hapo mwaka 1343 Hijria Shamsia baada ya matukio ya umwagaji damu ya tarehe 15 Khordad mwaka 1342. Tarehe 12 Bahman mwaka 1357 Imam alirejea nchini akitokea Ufaransa na katika siku kama ya leo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasili katika mji mtakatifu wa Qum na kuishi huko.

Miezi kadhaa baadaye Imam Ruhullah Khomeini alihamia Tehran kutokana na udharura wa kuongoza harakati ya Mapinduzi.

Imam Khomeini