Jumamosi, 4 Machi, 2023
Leo ni Jumamosi 11 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 4 Machi 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1411 iliyopita, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, maarufu kwa jina la Ali Akbar, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein (as) na mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) mjini Madina. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake, Mtume Mtukufu (saw), alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake, Imam Ali (as), na baba yake, Imam Hussein (as). Ali bin Hussein alikuwa maarufu kwa jina la Ali al Akbar yaani Ali Mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali. Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma za utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo inatambiliwa nchini Iran kwa jina la Siku ya Vijana. ***

Siku kama ya leo miaka 915 iliyopita alifariki dunia, Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 467 Hijiria, na akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Aidha vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi.
Katika siku kama ya leo miaka 167 iliyopita mji wa Herat ulioko kaskazini-magharibi mwa Afghanistan ya sasa ulijitenga na Iran. Mji huo na maeneo ya jirani yalikuwa sehemu ya Irani. Baada ya kupanuka ushawishi na uwepo wa Waingereza katika Bara Hindi, nchi hiyo ilichochea kujitenga kwa Herat na Iran na baadaye watawala wa Kabul na Kandahar walilivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la Herat. ***
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani, mmoja wa maulama wachaji-Mungu wakubwa na mwanamapambano. Alizaliwa mwaka 1262 Hijiri mjini Isfahan, Iran. Baba na babu yake, walikuwa kati ya maulama wakubwa wa eneo ambapo naye pia alipata kusoma kutoka kwao elimu mbalimbali. Baada ya Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani kusoma baadhi ya masomo ya kidini kutoka kwa baba yake (yaani Muhammad Baqir Agha Najafi) alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo mjini hapo. Miaka mitano baadaye alirejea mjini Isfahan na kuwa mmoja wa maraajii wakubwa wa mji huo. Aidha mbali na masuala ya kidini, Ayatullah Muhammad Taqi Agha Isfahani alikuwa mwanaharakati mzuri wa masuala ya kisiasa. Katika uwanja huo, msomi huyo alipambana vikali na upotoshaji wa kifikra na kiutamaduni na kadhalika ufisadi wa watawala dhalimu wa wakati huo. Wakati huo huo aliongoza harakati za kimapambano dhidi ya ukoloni wa kigeni hususan Uingereza. Ameacha athari mbalimbali vikiwemo vitabu vya 'Fiqhul-Imaamiyyah' 'Bahth Fii Wilaayati Haakimul-Faqih' na 'Dalaailul-Ahkam.' ***