Jumapili, 5 Machi, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 12 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria sawa na tarehe 5 Machi 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 946 iliyopita aliaga dunia Hassan bin Hafiz Ghassani mpokeaji hadithi na tabibu mashuhuri wa Andalusia, sehemu ya Uhispania ya leo. Ghassani alikuwa mwanafasihi mahiri na tabibu mweledi. Aidha alikuwa na hati za kuvutia sana na mwenye kipaji kikubwa cha kutunga mashairi. Kitabu cha Tamjidul Muhmal ni miongoni mwa athari muhimu za msomi huyo wa Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, sawa na tarehe 5 Machi 1827 alifariki dunia Alessandro Volta, mtaalamu wa fizikia wa Italia akiwa na umri wa miaka 83. Sambamba na kufundisha katika chuo kikuu, Volta alikuwa akifanya uhakiki na alifanikiwa kutengeneza chombo cha kupimia kiwango cha umeme Electrometre. ***
Tarehe 5 Machi miaka 70 iliyopita alifariki dunia Joseph Stalin, kiongozi na dikteta wa Urusi ya zamani. Stalin alizaliwa mwaka 1879 nchini Georgia na alijiunga na mrengo wa kikomunisti baada ya kusoma fikra za mrengo huo. Joseph Stalin alipelekwa uhamishoni huko Siberia mwaka 1913 kutokana na harakati zake za kisiasa dhidi ya serikali ya wakati huo ya Urusi. Stalin alibakia huko hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Urusi mwaka 1917. Alipata vyeo vya ngazi za juu wakati wa uongozi wa Lenin na alishika uongozi wa nchi hiyo akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri baada ya kufariki dunia Lenin. Mwaka 1927 Stalin aliwafutilia mbali wapinzani wake ndani ya chama na kuwa kiongozi asiye na mpinzani katika Chama cha Kikomunisti. Joseph Stalin aliendelea kuwafuta na kuwaangamiza bila ya huruma wapinzani wake ndani na nje ya chama hicho. ***
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu wa zamani wa Iran na kiongozi wa harakati ya kutaifishwa sekta ya mafuta na kuwa mali ya taifa.. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni. Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu. Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo. ***
Tarehe 5 Machi miaka 10 iliyopita alifariki dunia rais wa zamani wa Venezuela, Hugo Chavez. Chavez aliyezaliwa tarehe 28 Julai mwaka 1954 alikuwa rais wa 64 wa nchi ya Venezuela. Alitambulika kama kinara wa "Mapinduzi ya Kibolivari" na alipata umashuhuri kwa siasa zake za demokrasia ya kisoshalisti, kupinga utandawazi wa kileberali na sera za nje za Marekani na kuziunga mkono Iran na Palestina. Hugo Chavez aliaga dunia mwezi Machi mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 58 kutokana na maradhi ya saratani. ***
Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita alifariki dunia mbunifu wa E-mail yaani baruapepe, Ray Tomlinson. Tomlinson ambaye mwaka 1971 alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja ya uhakiki kama mhandisi huko Boston nchini Marekani alianzisha mfumo wa awali wa E-mail katika mtandao wa Arpanet yaani nakala ya kwanza na intaneti. Mtaalamu huyo kwa hakika alituma baruapepe ya kwanza kabisa kwa mtindo wa kisasa. Ray Tomlinson alifariki dunia katika tarehe aliyozaliwa akiwa na umri wa miaka 75 kutokana na ugonjwa wa kiharusi. ***