Mar 06, 2023 22:59 UTC
  • Jumanne, tarehe 7 Machi, mwaka 2023

Leo ni Jumanne tarehe 14 Shaaban mwaka 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Machi mwaka 2023.

Katika siku kama ya leo miaka 749 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas. Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli. Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.

Thomas Aquinas

Tarehe 7 Machi miaka 258 iliyopita alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa sanaa ya upigaji picha. Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833.

Nicephore Niepce

Siku kama hii ya leo miaka 87 iliyopita vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw, eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo.

Adolph Hitler

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, aliuawa Ali Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi. Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi, ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake.

Ali Razmara