Mar 07, 2023 22:52 UTC
  • Jumatano, tarehe 8 Machi, mwaka 2023

Leo ni Jumatano tarehe 15 Shaaban 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Machi Machi mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1189 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (as) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra Kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa, Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Ferdinand Marcos

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Abdur Rahim Rabani Shirazi, fakihi na mwanamapambano asiyechoka. Alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Shirazi moja ya miji ya kusini mwa Iran. Mwaka 1342 Hijria Shamsia, Abdur Rahim Rabani Shirazi alianza kushiriki katika harakati za mapambano dhidi ya utawala wa wakati huo wa Shah na kudumu katika harakati hizo. Mara kadhaa alikamatwa na kutiwa jela sambamba na kubaidishwa katika maeneo mbalimbali. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Majlisi ya ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran). Alimu huyu aliutumia umri wote kwa ajili ya kuuhudumia Uislamu na Waislamu.

Ayatullah Abdur Rahim Rabani Shirazi

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Machi 1985, ulitokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa garini mjini Beirut, Lebanon ambapo watu wasiopungua 45 waliuawa na wengine 175 kujeruhiwa. Mlipuko huo ulitokea karibu na msikiti unaotumiwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mlipuko huo ulifuatilia mlipuko mwengine mkubwa zaidi uliotokea mwaka 1983, ambapo watu wasiopungua 61 waliuawa kusini mwa bandari ya Tyre, nchini Lebanon. 

Leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.