Ebola yazidi kuwa tishio katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mlipuko wa maradhi ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unasambaa zaidi ya juhudi zinazochukuliwa za kuudhibiti huku zaidi ya watu 2,000 wakiambukizwa na zaidi ya 750 wakiwa wameaga dunia.
Ni takribani majuma mawili sasa tangu mlipuko wa Ebola wa aina ya Bundibugyo uanze tena mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hata hivyo badala ya hali kutulia, ugonjwa huo umeendelea kusambaa kwa kasi katika majimbo matano huku idadi ya maambukizi na vifo ikiongezeka kila siku.
Mkurugenzi wa Operesheni wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, Bruno Michon, anasema mlipuko huo unaenda kasi kuliko uwezo wa kuudhibiti. "Sasa ni miezi miwili tangu mlipuko huu uanze. Tangu tarehe 15 Mei, tumeshuhudia hali mbaya sana, na sasa imefikia kiwango cha kutisha. Tunakaribia visa 2,000 vilivyothibitishwa rasmi na zaidi ya vifo 700. Mlipuko huu sasa umeenea katika majimbo matano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa."
Ripoti zinazotolewa zinataja mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Haut-Uele na Tshopo kuwa ndiyo maeneo yaliyoathirika. Ni mara ya kwanza kwa mikoa ya Haut-Uele na Tshopo kujumuishwa katika ripoti ya hali ya kitaifa. Uchunguzi wa kitabibu unaonyesha kuwa visa vilivyogunduliwa katika mikoa hiyo miwili vina uhusiano wa kimaambukizi na kitovu cha mlipuko huo katika mkoa wa Ituri, kutokana na muingiliano na mienendo ya idadi ya watu.
Mlipuko huu wa sasa wa Ebola, ambao ni wa 17 kuwahi kuikumba nchi hiyo, ulitangazwa rasmi mnamo Mei 15 na umekuwa ukijikita zaidi katika mkoa wa Ituri, huku visa vingine vikiripotiwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Ugonjwa huu wa virusi, ambao mara nyingi husababisha mauti, huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili (damu, mate, nk) kutoka kwa watu au wanyama walioambukizwa. Dalili zake kuu ni pamoja na homa kali, kutapika,