Kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya Ebola DRC huku maambukizi yakienea
Kituo kikubwa zaidi cha matibabu ya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kimefunguliwa wiki hii na wadau wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha mwitikio dhidi ya mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo unaoendelea kuenea kwa kasi katika jimbo la Ituri, mashariki mwa taifa hilo.
Kituo hicho kipya kilichojengwa eneo la Rwankole, takribani kilomita tano kutoka makazi ya wakimbizi ya Kigonze, jimboni Ituri, kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 100 na kinatarajiwa kuongeza uwezo wa mfumo wa afya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa.
Hayo yanajiri wakati ambao jana Jumatano, mamlaka za afya DRC zilizitaka taasisi husika kuongeza kasi ya mwitikio dhidi ya mlipuko wa Ebola nchini humo baada ya idadi ya vifo katika mlipuko wa sasa kuzidi 1,750 huku maambukizi yakiendelea kusambaa.
Mlipuko huu wa karibuni wa Ebola nchini Kongo sasa umekuwa wa pili kwa ukubwa duniani kwa idadi ya maambukizi yaliyorekodiwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi punde ya tathmini ya hali, angalau visa 3,874, vikiwemo vifo 1,751, vimerekodiwa tangu mlipuko huo ulipotangazwa katikati ya mwezi Mei.
Kiwango cha vifo kwa walioambukizwa kwa sasa kimefikia asilimia 45.1.
Wagonjwa 717 kwa sasa wako katika vituo vya kutengwa au hospitalini, huku watu 749 wakiripotiwa kupona.
Kituo cha Operesheni za Dharura za Afya ya Umma nchini humo kimetoa wito wa kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa pamoja na uratibu wa pamoja, ili kupunguza hatari ya Ebola kuenea zaidi kutokana na kiwango kikubwa cha watu kusafiri na kuhama kutoka eneo moja hadi jingine.
Virusi hivyo vimeathiri majimbo matano ambayo ni Haut-Uele, Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tshopo.
Ituri ndiyo inayobaki kuwa kitovu cha mlipuko huu wa maradhi unaosababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo.