Alkhamisi, tarehe 9 Machi, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Shaaban 1444 Hijria sawa na tarehe 9 Machi 2023.
Siku kama ya leo miaka 569 iliyopita, sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia, Amerigo Vespucci. Kwa mara nne Vespucci alifanya safari kuelekea ardhi zisizojulikana ambazo hadi wakati huo zilikuwa hazijawa na majina ambapo kutokana na jina lake (Amerigo), ardhi hizo zikaitwa kwa jina hilo yaani ‘Amerika, au Marekani’. Ni kwa ajili hiyo ndio maana watu wengi wakamtaja Americo kuwa mvumbuzi asili wa Marekani. Americo Vespucci alifariki dunia mwaka 1512 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, aliuawa Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu. Sayyid Jamaluddin mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin al Afghani, alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika taaluma za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi. Sayyid Jamaluddin Assadabadi alikuwa mmoja wa waanzilishi wa fikkra ya umoja wa Kiislamu na mmoja wa wapinzani wakubwa wa ushawishi wa kikoloni katika nchi za Kiislamu. Alifanya jitihada kubwa za kuyaamsha mataifa ya Kiislamu kwa kuchapisha magazeti ya Al Urwatul Wuthqa mjini Paris na Dhiyaul Khafiqin mjini London. Vilevile alieneza mawazo za kupigania uhuru miongoni mwa watu kwa hotuba zake za hamasa, na kwa sababu hiyo alikabiliwa na uadui na wakoloni na tawala dhalimu. Hatimaye, Sayyid Jamaluddin Asadabadi alikwenda kwenye mji mkuu wa utawala wa Kiothmania, Istanbul, baada ya kuandamwa na kufuatiliwa huko Ulaya. Hata hivyo Abdul Hamid, mfalme wa utawala huo alimpa sumu na kumuua shahidi.
Tarehe 9 Machi mwaka 1992, Menachem Begin mmoja kati ya waasisi wa utawala haramu wa Israel na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa nchini Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baada ya kuhamia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, sawa na mwaka 1942 akateuliwa kuwa kamanda wa taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada kwa jina la "Irgun." Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyokuwa ikitekeleza mauaji dhidi ya raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao. Alikuwa katili sana dhidi ya raia wa Palestina kiasi kwamba David Ben Gorion ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa utawala haramu wa Israel alisema kuwa Begin ndiye Hitler wa kweli.
Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.