Jumapili, 12 Machi, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 19 Shaaban 1444 Hijria mwafaka na tarehe 12 Machi 2023 Miladia.
Miaka 1438 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, vilitokea vita vya Bani Mustalaq. Bani Mustalaq lilikuwa kabila miongoni mwa makabila ya Khaza'ah ambalo lilihamia katika vitongoji vya Makka miaka mingi iliyopita. Viongozi wa kaumu hiyo walikuwa wakiabudu na kueneza ibada ya masanamu huko Makka. Bani Mustalaq walijiandaa kupigana vita na Waislamu baada ya Uislamu kushika madaraka huko Madina. Kwa msingi huo, Mtume Muhammad (saw)aliingia vitani pamoja na wafuasi wake kadhaa na kutoa pigo kubwa kwa kabila hilo. ***
Miaka 169 iliyopita katika siku kama hii ya leo mkataba wa kihistoria wa Constantinople (Istanbul) ulitiwa saini baina ya Ufaransa, Uingereza na utawala wa kifalme wa Othmaniyyah. Baada ya nchi hizo tatu kutia saini mkataba huo dhidi ya sera za kujitanua za Urusi ya zamani huko Ulaya, zilipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata ushindi dhidi ya Urusi katika vita vya Crimea. **

Miaka 98 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Sun Yat-sen mwanamapinduzi na Rais wa Kwanza wa China. Sun Yat-sen anayejulikana kama baba wa taifa la China alizaliwa mwaka 1866 huko Nanlang China. Mwaka 1892 alijiunga na Chuo Kikuu na akiwa na umri wa miaka 26 alifanikiwa kupata shahada ya udaktari. Uwanja na mazingira ya Sun Yat-sen ya kuanzisha harakati zake za kisiasa yaliandaliwa baada ya Japan kuishambulia China mnamo mwaka 1894. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanzisha harakati zake dhidi ya mfumo wa kifalme wa Manchu. Baada ya harakati hiyo kushindwa alikimbilia nje ya nchi. Mwaka 1905 alirejea China na kuanzisha Muungano wa Wanamapinduzi wa China lengo likiwa ni kuleta demokrasia katika nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1911 utawala wa familia ya kifalme ya Manchu ulifikia tamati baada ya kupinduliwa. Tukio hilo lilipelekea kutangazwa mfumo wa Jamhuri nchini China na Sun Yat-sen alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China. ***
Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Machi 1930 ilianza harakati kubwa ya uasi iliyoongozwa na Mahatma Gandhi, kiongozi wa mapambano ya kupigania uhuru wa India. Harakati hiyo kubwa ambayo iliwashirikisha wazalendo na wapigania uhuru wa India, ilifanyika kwa shabaha ya kukabiliana na maamuzi mapya ya serikali ya kikoloni ya Uingereza kuhusu ongezeko la ushuru wa chumvi. Katika kukabiliana na sheria hiyo ya kidhalimu, Mahatma Gandhi na wenzake elfu 78 walianza kutayarisha chumvi kutoka maji ya baharini. Wakoloni wa Uingereza walikabiliana na harakati hiyo kwa kuwatia nguvuni makumi ya maelfu ya Wahindi na kuwatia korokoroni. Hali hiyo ilisababisha ghasia na vurugu katika idara za serikali. Mapambano hayo ya Mahatma Gandhi yaliilazimisha serikali ya kikoloni ya Uingereza kusalimu amri na kulegeza misimamo yake. ***
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita sawa na tarehe 12 Machi 1968 nchi ndogo ya Mauritius iliyoko kusini mwa Afrika ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Waholanzi waliingia Mauritius katika karne ya 17 na wakafuatiwa na Wafaransa karne moja baadaye. Mwaka 1814 Waingereza walikivamia kisiwa cha Mauritius na kukiunganisha na makoloni yao. Kisiwa hicho kina ukubwa wa kilomita mraba elfu mbili hivi na jamii ya zaidi ya watu milioni moja. ***
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita yaani tarehe 21 Esfand 1363 Hijria Shamsia, Ayatullah Mahmoud Ansari Qomi, mmoja wa Maulamaa mashuhuri wa Tehran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1300 katika mji mtakatifu wa Qom ulioko kusini mwa mji mkuu Tehran. Baba yake aliaga dunia wakati yeye akiwa na umri wa miak 10 na kaka zake kuchukua jukumu la kumlea ambapo ndi kipindi hicho pia alisoma masomo ya msingi ya Kiislamu. Baadaye alielekea Najaf Iraq na kunufaika na bahari ya elimu ya waalimu mahiri wa zama hizo. Ansari Qomi alifanikiwa kupata ijaza ya kunukuu hadithi pamoja na Ijtihadi kutoka kwa Maulamaa kadha wa Iran na Iraq. Mwanazuoni huyu ameacha pia athari ya vitabu muhimu hasa katika elimu ya fikihi, usul na tafsiri. ***