Mar 16, 2023 00:11 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 16 Machi, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Shaaban 1444 Hijria, sawa na tarehe 16 Machi 2023

Siku kama ya leo Miaka 1140 iliyopita, Abu Muhammad Hassan bin Ali Utrush aliyepewa lakabu ya Nassir Kabir na ambaye alikuwa mwanazuoni na mwanapambano mashuhuri katika wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw) aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina na kubaidishiwa mjini Samarra huko kaskazini mwa mji wa Baghdad nchini Iraq na wafalme wa Bani Abbas akiwa na idadi kadhaa ya watu wa ukoo wa Mtukufu Mtume akiwemo Imam Hassan Askari (as) na baba yake Hassan Utrush. Alijifunza elimu za kidini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa mwanazuoni mashuhuri katika elimu hizo. Alijishughulisha na masuala ya kisiasa pia ambapo alikuwa na nafasi muhimu katika kipindi cha mapambano na kusimamishwa dola la Maalawi huko Tabarestan kaskazini mwa Iran. Alifanya juhudi kubwa za kueneza dini ya babu yake, Mtume Mtukufu (saw) ambapo aliwaingiza makumi ya maelfu ya watu katika dini tukufu ya Uislamu. Aliandika pia vitabu vingi katika uwanja huo vikiwemo vya al-Basit, Tafsir al-Utrush na al-Imamatul Kabir.

Abu Muhammad Hassan bin Ali Utrush

Katika siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake. Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo. Katika kipindi chote cha masomo, Parvin I’tisami alikuwa mwanafunzi bora shuleni. Safari zote alizifanya akiwa pamoja na baba yake na kujifunza mambo mengi katika safari hizo. 

Parvin I’tisami

Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi. Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler. 

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi mwaka 1909.

Bi Selma Lagerlof

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa.  Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt  alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon. Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt  aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo  akiwa na umri wa miaka 60.

Kamal Fouad Jumblatt 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Mahdi Bakeri mmoja wa makamanda mashujaa na wenye tadibiri katika kipindi cha kujihami kutakatifu wanananchi wa Iran mbele ya hujuma na mashambulio ya kichokozi ya jeshi la dikteta  wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein alikufa shahidi. Alizaliwa katika mji wa Miandoab kaskazini magharibi mwa Iran na mama yake alifariki dunia wakati yeye akiwa mtoto mdogo. Kaka yake naye kutokana na kuonyesha upinzani dhidi ya utawala dhalimu wa Shah aliuawa na makachero wa utawala huo. 

Mahdi Bakeri

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, utawala wa Baath nchini Iraq uliushambulia bila huruma na kwa mabomu ya kemikali za sumu mji wa Halabja wa wakazi wa Kikurdi huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa kutumia makumi ya ndege za kivita. Hujuma hiyo ilianza baada ya kushindwa kupambana na wapiganaji Waislamu wa Iran na wa Kikurdi wa huko Iraq, na katika upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabja waliwakaribisha wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo wa Saddam Hussein dhidi yao. Raia elfu tano wasio na hatia waliuawa kutokana na kuvuta gesi ya sumu huko Halabja. Hata hivyo nchi za Magharibi hazikuchukua hatua yoyote kwa jinai hiyo kubwa na ya kutisha.

Halabja