Mar 25, 2023 10:37 UTC
  • Jumamosi, 25 Machi, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 3 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria, mwafaka na tarehe 25 Machi 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1031 ilyopita inayosadifiana na tarehe 3 Ramadhani 413 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Nu'uman maarufu kwa lakabu ya Sheikh Mufiid, faqihi, mtaalamu wa elimu ya Hadithi, Qurani Tukufu na historia ya Kiislamu. Sheikh Mufid alikuwa hodari na mwanafikra aliyepevuka, kwani aliweza kujibu masuala ya kifiqihi kwenye midahalo kulingana na madhehebu yoyote aliyotakiwa kufanya hivyo. Kutokana na uhodari wake huo, maulamaa wengi wa Kiislamu katika zama hizo walimpa lakabu ya Mufiid. Sheikh Mufiid ameandika vitabu vingi miongoni mwa hivyo, ni al Kalaam Fii Dalaailil Quran', al Arkaan' na˜Kashful Saraair'. ***

Shekhe Mufid

 

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, mkataba wa kuasisi Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya au kwa jina jingine Soko la Pamoja la Ulaya ulisainiwa huko Roma mji mkuu wa Italia kati ya wawakilishi wa nchi mbalimbali za bara hilo. Jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuasisi umoja wa forodha kati ya nchi wanachama ili kufuta ushuru wa bidhaa na baada ya hapo, ubadilishanaji wa bidhaa, nguvu kazi, vitega uchumi na huduma nyinginezo pia ukawa huru kati ya nchi wanachama. Jumuiya hiyo ilikuwa utangulizi wa kuundwa Umoja wa Ulaya mwaka 1992. ***

Umoja wa Ulaya

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Mfalme wa wakati huo wa Saudi Arabia, Faisal bin Abdulaziz, aliuawa na mwana wa ndugu yake mwenyewe, Faisal bin Saaid bin Abdulaziz. Faisal bin Saaid alifanya mauaji hayo akilalamikia kupunguzwa kwa mshahara wake. Japokuwa hitilafu katika kizazi cha wafalme wa Saudi Arabia zimekuwepo siku zote na zimekuwa zikipamba moto mara kwa mara lakini mauaji ya Mfalme Faisal yalikuwa ya kwanza ya mfalme wa nchi hiyo kutokana na hitilafu kama hizo. Muuaji wa Mfalme Faisal pia alikatwa kichwa mbele ya umati wa watu tarehe 18 Juni mwaka 1975. Baada ya Faisal, Khalid mwana mwingine wa Abdulaziz alishika kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. ***

Faisal bin Abdulaziz

 

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, vikosi vamizi vya Marekani ambavyo mwezi Disemba 1992 viliwasili nchini Somalia kwa kisingizio cha kukomesha uasi nchini humo, hatimaye vililazimika kuondoka katika nchi hiyo baada ya kushindwa vibaya na bila ya kutarajia. Mwaka 1991 makundi mbalimbali ya Somalia yalimpindua dikteta wa nchi hiyo Muhammad Siad Barre. Hata hivyo makundi hayo yalishindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na mkwamo huo wa kisiasa ukapelekea kuzuka vita vya ndani nchini humo. Marekani ilituma wanajeshi wake huko Somalia katika fremu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kulinda maslahi yake nchini humo, kutokana na nafasi muhimu ya Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika. Jeshi la Marekani lilikabiliwa na mapambano makali ya Wasomali na kupoteza askari karibu 100. ***

 

Tags