Jumatatu, Juni 20, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 14 Ramadhani 1437 Hijria sawa na Juni 20, 2016.
Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini.
Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na K na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.
Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo. Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan. Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo lakini Marekani imebakisha kambi yake ya kijeshi katika kisiwa hicho.
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika taaluma ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha Rishta ulitikisa mikoa ya Gilan na Zanjan huko kaskazini mwa Iran na kusababisha hasara kubwa ya mali na nafsi.
Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa mji wa Rudbar na ulisababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 50 na kujeruhi wengine zaidi ya elfu 60. Mtetemeko huo ambao uliwalazimisha watu nusu milioni kuwa wakimbizi pia ulisababisha hasara kubwa za kiuchumi.
Na tarehe 14 Ramadhani miaka 23 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili.
Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ililazimika kumshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!