Apr 04, 2023 22:38 UTC
  • Jumatano tarehe 5 Aprili 2023

Leo ni Jumatano tarehe 14 Ramadhani 1444 Hijria sawa na Aprili 5 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Ramadhani mwaka 67 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abu Ubaida al Thaqafi, kiongozi wa harakati ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, akilinda dini tukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar al Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, na hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi katika siku kama hii ya leo.

Kaburi la Mukhtar bin Abu Ubaida al Thaqafi

Siku kama ya leo miaka 438 iliyoyopita yaani 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Uhispania hapo mwaka 1609.

Mji wa Harlem nchini Uholanzi

Tarehe 5 Aprili 229 iliyopita, aliuawa Georges Danton mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mzuri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kimtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa.

Georges Danton

Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi hayo, tarehe 4 Aprili, yalianza kufanya mashambulio makubwa na kuwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee katika kipindi cha siku mbili. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.

Mashambulizii ya Israel dhidi ya watu wa Gaza