May 15, 2023 10:01 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (17)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 17 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 17.

Wasikilizaji wapenzi, siku moja Imam Ali AS aliulizwa kuhusu kauli hii ya Mtume (SAW) ambaye amenukuliwa akiwaambia Waislamu: Badilisheni rangi za nywele zenu nyeupe ili msiwe kama Mayahudi. Imam alijibu kwa kusema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alisema hayo wakati Waislamu walipokuwa ni wachache, lakini sasa idadi ya Waislamu ni kubwa, hivyo kila mtu anaweza kufanya anavyopenda.

Hikma ya 17 ya Nahjul Balagha mpenzi msikiliizaji inahusiana na swali na udadisi wa mmoja wa wafuasi wa Imam Ali AS, ambaye alitaka kujua sababu ya kwa nini Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akiwaambia maswahaba wake watie rangi nywele zao na wasiwe kama Mayahudi wasiopaka rangi nywele zao. Lakini baada ya miaka mingi ya kutangulia mbele ya haki Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Ali AS ikawa hafuati amri hiyio ya Bwana Mtume SAW wakati yeye ndiye mtu aliyestahiki zaidi kufuata amri na Hadith za Mtume Muhammad SAW ili watu wengine nao waweze kuendeleza sunna hizo. Kwa hiyo, alikwenda kwa Imam na kumuuliza; hadithi ya Bwana Mtume SAW aliyenukuliwa akisema: Badilisheni uzee wenu kwa pambo la rangi ili msifanane na Mayahudi, ina maana gani?

Imam Ali AS alitambua kwamba mtu huyu ilikuwa mambo yamemchanganyikia mpaka akafikia kufikiri kwamba kwa vile Ali AS, ni wasii na khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, alikuwa hafanyi kama inavyosema sunna ya Mtume. Imam alimjibu mtu huyo kwa kumwambia: Ndugu yangu! Zama ambazo Bwana Mtume (SAW) alikuwa akiwahimiza Masahaba wake kutekeleza sunna hiyo ilikuwa ni zama ambazo Masahaba wa Mtume walikuwa wachache na dhaifu mbele ya maadui. Kwa hiyo, hatua yake wakati huo ya kuwaamrisha Masahaba wake wapake rangi nywele zao, ilikuwa ni mbinu ya kisaikolojia katika kuendesha mambo kwa hikma. Kwa sababu kwa kawaida uzee ni ishara ya udhaifu na Bwana Mtume hakutaka Waislamu waonekane dhaifu. Alikuwa akiwaamrisha Masahaba wake wapake rangi nywele zao kuondoa sura ya uzee na hilo lilikuwa na taathira kubwa za kisaikolojia mori na moyo wa kusimama imara kuupigania Uislamu. Adui alipowaona Waislamu alisema katika nafsi yake, ikiwa wazee wao wako hivi, basi vijana wao watakuwa imara zaidi, watakuwa na mori na dhamira kubwa kiasi gani ya kuupigania Uislamu?!? Ni kwa sababu hiyo ndio maana Mtume Mtukufu SAW aliwaamrisha Masahaba wake kupaka rangi nywele zao. Pia na ili maadui, Mayahudi na washirikina, wasijue uhakika wa hikma na amri yake hiyo, Mtume Mtukufu alifungamanisha sunna hiyo na Mayahudi ambao walikuwa hawafuati sunna hiyo. Hivyo aliwataka Waislamu wapake rangi nywele zao ili wasifanane na Mayahudi. Imam Ali AS aliendelea kumwambia mtu huyo kwamba: Lakini sasa Waislamu wana nguvu, wametwaa madaraka huku maadui zao wakiwa wamedhoofika. Hivyo kupaka rangi nywele nyeupe hakuongezi chochote katika mamlaka na nguvu za Waislamu. Hivyo mtu yeyote anayetaka kupaka nywele zake na afanye hivyo na yeyote ambaye hataki anaweza kuacha sunna hiyo.

Hikima ya 17 ya Nahjul Balagha ni kama ifuatavyo:

وَ سُئِلَ (علیه السلام) عَنْ قَوْلِ الرَّسُولِ (صلی الله علیه وآله) "غَیِّرُوا الشَّیْبَ وَ لَا تَشَبَّهُوا بِالْیَهُودِ"؟ فَقَالَ (علیه السلام): إِنَّمَا قَالَ ذَلِکَ وَ الدِّینُ قُلٌّ، فَأَمَّا الْآنَ وَ قَدِ اتَّسَعَ نِطَاقُهُ وَ ضَرَبَ بِجِرَانِهِ؛ فَامْرُؤٌ وَ مَا اخْتَارَ

"Na aliulizwa Imam Ali AS kuhusu kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW aliposema: "Badilisheni mvi zenu ili msifanane na Mayahudi. Imam Ali alijibu kwa kusema: Mtume hakusema hayo ila wakati ambapo Waislamu walikuwa wachache. Lakini hivi sasa mamlaka ya Uislamu imetanuka na imekuwa kubwa na dini imeimarika, aendeleze sunna hiyo yeyote apendaye.