May 26, 2023 11:16 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (68)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo.

Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri. 

Kipindi chetu kilichopita kilimzunguzia Shekhe Fadhlullah Kojuri. Tulisema kuwa, Fadhlullah Kojuri mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Fadhlullah Nouri alizaliwa 1259 mwafaka na 1843 Miladia katika Wilaya ya Kojur kwenye mji wa Nur ulioko katika mkoa wa Mazandaran Iran. Moja ya hatua muhimu za alimu huyu ni himaya na uungaji mkono wake kwa harakati ya kupigania katiba nchini Iran. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 68 kitamzungumzia msomi na mwanazuoni mwingine mahiri na mashuhuri ambaye si mwingine bali ni Mirza Habibullah Rashti. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki juma hili.

Sheikh Murtadha Ansari

 

 

Mwanafunzi mwingine maalumu wa Sheikh Murtadha Ansari ni Mirza Habibullah Rashti. Huyu ni mmoja wa wanafunzi ambao Shekhe Murtadha Ansari hakuwa akianza kufundisha mpaka awe amewasili darasani.

Mahudhurio ya wanafunzi maalumu mfano wa Habibullah Rashti katika darsa na somo la Shekhe Murtadha Ansari yalikuwa na umuhimu mkubwa kwa mwalimu huyu, kwani alikuwa akitambua kwamba, katika mustakabali wanafunzi hawa watakuwa na majukumu makubwa kiasi gani.

Sahib Jawahir

 

Habibullah Rashti alizaliwa 1234 Hijria katika mji wa Gilan Iran katika eneo linalojulikana kwa jina la Amlash. Mababu zake walikuwa na asili ya Quchan na baba yake Muhammad Ali Quchani Gilani alikuwa akihesabiwa kuwa mmoja wa watu na shakhsia mahiri na wakubwa wa Gilan.

Habibullah Rashti alianza kujifunza elimu katika nyumba ya baba yake na alianza  kujifunza maneno ya Mwenyezi Mungu yaani Qur’ani. Akiwa na umri wa miaka 12 Habibullah Rashti alifunga safari na kwenda Rasht kwa minajili ya kujiendeleza zaidi kielimu.

Tangu katika kipindi cha ujana wake, Habibullah Rashti alikuwa akifuatilia na kupigania uadilifu. Hakuwa na umri usiozidi miaka 18 lakini alikuwa akisimama kidete mbele ya shakhsia wakubwa wa Rasht kwa ajili ya kuhakikisha dhulma aliyotendewa mtu inaondolewa na anafanyiwa uadilifu. Hata hivyo kutokana na umri wake mdogo, mawaidha na mahubiri yake hayakuwa na natija, hivyo akaamua kuondoka na kuuacha mji huo akiwa amechoshwa na dhulma iliyokuwa ikifanywa huku waliomzungumka wakinyamazia kimya dhulma hiyo.

Baba yake alifuatana naye hadi katika mji wa Qazvin na huko alimkabidhi mwanawe huyo kwa mwalimu wa ngazi ya juu aitwaye Abdul Karim Iravani ili amfundishe somo la fikihi na Usul. Habibullah akiwa Qazvin alioa akiwa angali kijana mdogo na kama alivyokuwa mwalimu wake, naye pia aliishi maisha ya kujinyima na kuipa mgongo dunia na akauchagua uchamungu kuwa njia yake ya maisha na akaendelea hivyo hadi mwishoni mwa umri wake.

 

 

Baada ya kumaliza masomo yake ya kidini, alirudi Amlash akiwa na umri wa miaka ishirini na mitano na alikuwa Marjaa wa kidini wa watu wa mji wake kwa miaka minne. Katika enzi za ujana wake, Mirza Habibullah Rashti, ingawa hakuhitaji masomo na mijadala kutokana na kubobea katika elimu, alifunga safari na kwenda Najaf kuhudhuria masomo ya Sahib Jawahir na kushiriki masomo ya Sheikh Murtadha Ansari.

Baada ya kuaga dunia Shekhe Murtadha Ansari, Umarjaa wa Kishia ukakabidhiwa kwa Mirza Shirazi Mkubwa. Hata hivyo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) ulikabidhiwa kwa Mirza Habibullah Rashti. Tabia na hali yake ya kujipamba na sifa ya kujinyima na kuipa mgongo dunia aliyoirithi kutoka kwa mwalimu wake wa Qazvin ni jambo ambalo lilimfanya Habibullah kutoingilia moja kwa moja masuala ya kijamii na kisiasa. Hata hivyo, daima alikuwa akiunga mkono Umarjaa wa Mirza Shirazi Mkubwa.

Wanafunzi wa Habibuullah Rashti kutoka kushoto: Muhaqqiq  Yazdi, Sheikh Fadhlullah Nouri na Ali Akbar Fal Asiri

 

Habibullah Rashti alikuwa akitambua vyema kwamba, ulimwengu wa Kiislamu unahitajia Marjaa mwanasiasa, na ndio maana daima alikuwa akisema, hii leo bendera ya Uislamu iko katika mabega ya Sayyid Muhammad Hassan Shirazi (Mirza Shirazi Mkubwa) na watu wote wanapaswa kuwa pamoja naye ili bendera hii isidondoke chini. Himaya na uungaji mkono wa Habibullah Rashti kwa Umarjaa wa Mirza Shirazi Mkubwa ulimfanya adui akose njia ya kutoa pigo kwa umoja wa Kishia.

Mbali na himaya na uungaji mkono wake wa kauli na matamko yake, aliwalea wanafunzi ambao kila mmoja alikuwa mithili ya kamanda wa Mirza Shirazi Mkubwa. Miongoni mwa wanafunzi hao ni Sayyid Ali Akbar Fal Asiri; mtu ambaye alifanya hima na idili isiyo na mithili katika utangulizi wa kutolewa fatuwa ya kuharamisha tumbaku. Sayyid Kadhim Yazdi au kama anavyojulikana kama Muhaqqiq Yazdi na Shekhe Fadhlullah Nouri ni miongoni mwa waliokuwa wanafunzi wake. Wawili hawa walikuwa na nafasi na mchango muhimu sana katika kupambana na upotoshaji wa mapinduzi ya kupigania katiba.

Mirza Habibuullah Rashti

 

Juhudi zake zilipelekea kupasishwa vipengee kamilishi vya katiba na hilo likapelekea kutambuliwa rasmi madhehebu ya Shia nchini Iran. Aidha natija ya juhudi za wasomi na Maulamaa hawa wawili ikawa ni kutambuliwa haki ya kidini ya Maulamaa ya kuwa na usimamizi kwa miswada na mambo yanayopasishwa na Bunge.

 

Mbali na kuwa na zuhdi na uchajimungu na kuishi maisha ya kawaida ambapo hata alifumbia macho hisa ya urithi wake, watu wote walikuwa wakimtambua kama mtu mwenye heshima, adabu na mwenye tawadhui na unyenyekevu na asiyependa kujikweza. Aidha Habibullah Rashti alikuwa na umakini maalumu katika kulinda na kutekeleza haki za baba na mama. Ni mashuhuri kwamba, baada ya baba na mama yake kuaga dunia Mirza Habibullah Rashti aliswali mara tatu Swala za kadha za wazazi wake hao. Mara ya kwanza kwa mujibu wa marajii aliokuwa akiwafuata na mara mbili zilizobakia ni kwa mujibu wa ijtihadi yake.

 

Katika uga wa uandishi wa vitabu mwanazuoni huyu ana athari na vitabu vingi pia. Hata hivyo athari yake muhimu zaidi ni “Badaiu al-Afkar” kitabu ambacho kinahusiana na masuala ya elimu ya Usul ambapo ndani yake amejadili na kuchambua kwa undani zaidi elimu hii. Kitabu hiki kilisambazwa  mwaka 1313 Hijria mjini Tehran, ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kuaga dunia mwanazuoni huyu. Mirza Habibullah Rashti aliaga dunia Alkhamisi ya tarehe 14 Jamad al-Thani 1312 Hijria katika mji wa Najaf Iraq.

Mwili wa mwanazuoni huyu umezikwa katika haramu ya Imam Ali ibn Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf Iraq. Baada ya kuaga dunia Habibullah Rashti aliyekuwa mwanazuoni mahiri na mtajika katika zama zake katika ulimwengu wa Kiislamu ulikumbwa na majonzi na simanzi kubwa. Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena juma lijalo saa na wakati kama wa leo. Basi hadi tutakapokutana tena wakati huo, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.