May 27, 2023 05:01 UTC
  • Sura ya Fat-h, aya ya 1-4 (Darsa ya 937)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 937. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 47 ya Muhammad, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 48 ya Al-Fat-h. Sura hii ambayo ina jumla ya aya 29, iliteremshwa baada ya Sulhu ya Hudaibiya ambayo ilifikiwa katika mwaka wa sita Hijria. Katika mwaka huo, Bwana Mtume Muhammad SAW akiandamana na idadi kubwa ya masahaba zake aliondoka Madina na kuelekea Makka kwa madhumuni ya kutekeleza ibada ya Umra, lakini washirikina waliwafungia njia katika eneo la Hudaibiya lililoko karibu na mji wa Makka na kutowaruhusu kuingia mjini humo. Mazunguumzo yaliyojiri hapo baina ya Waislamu na washirikina, hatimaye yaliishia kwa kusainiwa mkataba wa suluhu kati ya Bwana Mtume na wakuu wa washirikina ili kuandaliwa mazingira ya kuwawezesha Waislamu kuingia Makka miaka minne baadaye kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija. Wakati Bwana Mtume SAW na masahaba zake walipokuwa njiani kurejea Madina, ndipo sura hii ikateremshwa na kumpa mtukufu huyo bishara ya ushindi. Baada ya utangulizi huo mfupi tunaianza sasa darsa yetu hii kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا

Hakika tumekwishakupa Ushindi wa dhaahiri.

لِّيَغْفِرَ لَكَ اللَّهُ مَا تَقَدَّمَ مِن ذَنبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ وَيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَيَهْدِيَكَ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا

Ili Mwenyezi Mungu akughufirie makosa yako yaliyo tangulia na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoze katika Njia Iliyo Nyooka.

وَيَنصُرَكَ اللَّهُ نَصْرًا عَزِيزًا

Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu.

Aya hizi, ambazo ziliteremshwa baada ya Sulhu ya Hudaibiya, zimeitaja suluhu na mapatano hayo kuwa ni utangulizi wa ushindi muhimu kwa Uislamu na Waislamu katika siku za usoni. Sababu ni kuwa kabla ya hapo, kitu pekee walichokuwa wakiwaza washirikina ilikuwa ni kuwaangamiza Waislamu na wala hawakuwa wakiwapa thamani yoyote. Lakini miongoni mwa matunda ya mkataba wa Hudaibiya ilikuwa ni kutambuliwa rasmi Waislamu; na baada ya ushindi wa kuikomboa Makka, yaani ya Fat-hu ya Makka iliyopatikana katika mwaka wa nane Hijria, Waislamu walipata ushindi kamili dhidi ya washirikina.

Wakati alipodhihiri Bwana Mtume Muhammad SAW, umaarufu wa mila na desturi potofu na za mambo ya uzushi na khurafa za kijahilia ulipotea. Kutokana na kuletwa mafundisho ya Uislamu, mfumo wa kitabaka uliokuwepo katika jamii uliporomoshwa; na watu wote wa kila kabila, asili na rangi walitambuliwa kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu na walio ndugu baina yao. Lakini mbali na hayo, hatua ya Bwana Mtume SAW ya kupambana vikali pia na imani ya kuabudu masanamu na mila za kijahilia iliwachukiza sana vinara wa washirikina na halikuwa jambo la kuachiwa au kukubalika kirahisi. Na kwa sababu hiyo, walimchukulia Bwana Mtume SAW kuwa ni mtu mwasi kwa msimamo wake wa kuing'oa mizizi ya itikadi, mila na desturi potofu za kijahilia na kuleta mageuzi ya kimsingi ndani ya jamii. Kwa muhtasari tunaweza kusema, miongoni mwa matunda muhimu ya Sulhu ya Hudaibiya na baada yake Fat-hu ya Makka yalikuwa ni kufutwa kwa mila na desturi potofu za kijahilia. Mtume wa Allah aliasisi mfumo wa Kiislamu katika ardhi za Makka na Madina, mizozo ya kikabila ikamalizwa na moyo wa upendo na udugu ukatawala ndani ya jamii ya Waislamu. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, kujipanga na kuchukua maamuzi kwa kuzingatia uhalisia wa mambo, ndiko kunakoandaa mazingira ya kupata mafanikio. Kuwashinda maadui, si lazima kila mara kupatikane kwa njia ya vita na Jihadi; wakati mwingine suluhu na mapatano vinaandaa mazingira ya kupata ushindi dhidi ya maadui. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama sisi tutakuwa na hima na bidii ya kutimiza wajibu wetu pasi na kuhofu matokeo yake, Yeye mwenyewe Allah SWT atayakadiria mambo yaende kwa namna itakayoondoa yale tunayohofia na kupata yale tunayoyatarajia. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, maamuzi anayochukua Mtume kwa ajili ya kufanya suluhu au kupigana vita na maadui yanatokana na mwongozo na maelekezo ya Allah SWT na si kwamba mtukufu huyo anachukua hatua kwa kufuata matashi na matakwa ya nafsi yake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nne ya sura yetu ya Fat-h ambayo inasema:

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ ۗ وَلِلَّهِ جُنُودُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَلِيمًا حَكِيمًا

Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi Imani juu ya Imani yao. Na Mwenyezi Mungu ana majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima.

Katika tukio la Sulhu ya Hudaibiya, akthari ya Waislamu walikereka na kuhuzunika sana, wakahisi kama wameshindwa kwa sababu ya kutofanikiwa kuingia Makka na kutekeleza ibada ya Umra. Lakini kuteremshwa kwa sura hii na kutolewa bishara kwamba Waislamu watashinda katika siku za usoni, kuliwapa utulivu masahaba na kuzifanya imara zaidi imani zao kwa maneno ya Mtume wa Allah na ahadi alizowapa Yeye Mola. Ni wazi kwamba mtu anayeamini kuwa ulimwengu wote unaendeshwa kwa tadbiri, takdiri na makadirio ya Allah na kuitakidi kwamba vitu vyote vya maumbile mbinguni na ardhini vina uwezo wa kuwa askari wa Mwenyezi Mungu, katu huwa hajihisi ameshindwa, wala moyo wake hautishiki hata chembe kwa sababu ya nguvu, taadhima na makeke ya maadui. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, moja ya rehma na fadhila za Allah kwa waumini ni kuingiza utulivu na ushwari ndani ya nyoyo zao, kama ambavyo miongoni mwa adhabu na mateso anayowapa makafiri hapa duniani ni kuzijaza nyoyo zao woga na hofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, imani ina viwango na daraja na inaweza kila wakati kupanda na kushuka. Ukweli ni kwamba kujiri kwa matukio na kuzuka matatizo mbalimbali ni mtihani wa kuzipima imani za watu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kutafakari na kuamini juu ya uwezo, ujuzi na hekima ya Allah SWT na kwamba vitu vyote vya maumbile viko chini ya mamlaka na amri yake Mola, kunawapa waumini ushwari na utulivu maalumu wa ndani ya nafsi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 937 ya Qura'ni imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/