May 31, 2023 09:47 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (18)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 18 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 18.

(وَ قَالَ علیه السلام فِی الَّذِینَ اعْتَزَلُوا الْقِتَالَ مَعَهُ): خَذَلُوا الْحَقَّ وَ لَمْ یَنْصُرُوا الْبَاطِلَ 

(Na Imam Ali AS akasema kuhusu wale waliojitoa katika kupigana vita bega kwa bega na yeye kwamba): Wameipuuza haki na hawakuinusuru batili.

Vita vya Jamal, pamoja na msururu wake wote wa matukio ya kila namna kama ya kupenda ulimwengu, tamaa, ulafi wa madaraka, hila, upumbavu, ujanja na vitimbi vya kishetani, vilikuwa ni fitna kubwa ambayo ilikuwa mara ya kwanza kwa Waislamu kukumbana na fitna kama hiyo ambayo iliwafanya waanze kupigana vita vya umwagaji damu baina ya wao kwa wato. Kabla ya hapo, muda wote Waislamu walipoingia vitani walikuwa wanapigana na makafiri na washirikina. Lakini mara hii katika vita hivi vya Jamal, pande mbili zilizopigana zilikuwa ni za Waislamu wenyewe na kila upande ukidai ndio wenye haki. Tab'an miaka mingi nyuma kabla ya kutangulia kwake mbele ya Haki, Mtume Mtukufu SAW alikuwa ametabiri na kusisitiza kutokea vita hivi. Mtume alitumia neno naakithin yaani wavunja ahadi na kumwambia Imam Ali AS kwamba atapigana vita vya namna hiyo katika miaka ya usoni na ndivyo ilivyotokea. 

 

Watu walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya kupigana Jihadi dhidi ya waasi na wavurugaji usalama pamoja na wezi walioua na kupora watu na kuharibu miji mbali mbali hususan Basra. Wakati huo huo, wazee wanne walijitoa na walionyesha wasiwasi juu ya kupigana vita na Waislamu wengine. Miongoni mwa watu hao wakubwa walikuwa ni Abdullah bin Omar, Muhammad Muslimah na Osama bin Zayd. Watu hao walificha uongo wao nyuma ya tuhuma na wakasema kwamba tunatilia shaka uhalali wa vita hivi na tunaogopa mikono yetu isije ikatiwa doa na damu za Waislamu. Hapo Imam Ali (AS) aliamua kutumia hikma yake ya aina yake na kuwaambia: Nendeni majumbani mwenu na msijitokeze hadharani, msije mkaeneza kirusi cha shaka yenu kwa wengine. Kisha, kama ilivyoelezwa katika hikma ya kumi na tano; baada ya watu hao wanne kuondoka, walisema: "Si kila anayepatikana kwenye fitna, hustahiki kulaumiwa!" 

Wakati jeshi la Waislamu lilipojiandaa kutoka kwenda vitani, mtu mmoja aliyeitwa "Harith bin Hawt" aliingia shaka na wasiwasi moyoni baada ya kuathiriwa na maneno ya watu hao wanne. Rekodi za watu kama Talha na Zubair, ambao ndio waliokuwa waanzilishi wakuu wa fitna na vita vya Jamal, zilikuwa kama kizuizi kikubwa kwa "Harith bin Hawt" kilichofunga njia ya mawazo na fikra zake zote, kwani hakuguswa na misimamo yao isiyo sahihi tu lakini pia kupenda kwao kupewa fungu kubwa zaidi kuliko Waislamu wengine na kukengeuka kwao baia na utiifu kwa khalifa wa zama zao, yote hayo yanakumzindua. Ndio maana alimwambia Amirul-Muminin Imam Ali AS kwamba, Mimi, kama hawa wanne, sitashiriki katika vita hivi!

 

Imam Ali AS ambaye alijua kwamba watu wengi hawana uwezo wa kupambanua haki na batili katika matukio tata na fitna zilizojifunga kama hizo, hasa kutokana na kuwa na taarifa na welewa wa kutosha wa matukio, alimwambia Harith:

Ewe Harith! Usiangalie mambo kwa mtazamo finyu. Umeshindwa kuangalia mambo kwa kina na umakini ndio maana umechanganyikiwa na mambo! Umeshindwa kuijua haki ndio maana huwajui wenye haki, umeshindwa kuijua batili ndio maana huwajui walioko kwenye batili. Katika fitna ambazo upande mmoja uko kwenye haki na wa pili uko kwenye batili, hata kunyamaza kimya tu na kutoshiki kuihami haki, kwenyewe ni aina fulani ya kushirikiana na adui kupambana na haki. Naam! Tambua kuwa watu hao wameipuuza haki na hawakuinusuru batili.