Al-Ahly ya Misri wafalme wa soka barani Afrika 2023
Wydad Casablanca ya Morocco na Al Ahly ya Misri siku ya Jumapili waliendeleza vita vyao vya kutafuta mfalme wa klabu za soka barani Afrika, walipokutana katika mkondo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V mjini Casablanca.
Mafao wametwaa kombe hilo la kibara, licha ya mchuano huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Wenyeji Wydad walikuwa wa kwanza kucheka n nyavu kupitia goli la mapema la Yahya Attiatullah kunako dakika ya 27. Mafarao walitoka nyuma na kupata bao la kusawazisha, ambalo kimsingi lilikuwa la ushindi, katika dakika ya 78 ya mchezo kupitia kwa Muhammed Abdulmuumin.
Kwa sare hiyo Ahly wametwaa ushindi kwa jumla ya mabao 3-2.
Mechi ya kwanza katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo wikendi iliyopita ilimalizika kwa mabao 2-1 kwa upande wa Mafarao. Al Ahly, wametwaa taji la 11 la CAFCL lililoongeza rekodi, na la tatu katika muda wa misimu minne.