Jun 15, 2023 05:51 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (20)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 20 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni hikma ya 20.

أَقِیلُوا ذَوِی الْمُرُوءَاتِ عَثَرَاتِهِمْ، فَمَا یَعْثُرُ مِنْهُمْ عَاثِرٌ إِلاَّ وَ یَدُ اللَّهِ بِیَدِهِ یَرْفَعُهُ

Fumbieni macho utelezaji wa watu wenye murua, kwani hatelezi miongoni mwao mwenye kuteleza, ila mkono wa Allah humshika na kumnyanyua.

Mpenzi msikilizaji, Hikma ya 20 ya Nahj al-Balagha ina nasaha nzuri sana za kimaadili. Katika hikma hii, Imam Ali AS anaashiria utelezaji ambao baadhi ya wakati huwatokea watu waungwana, wenye murua na tabia nzuri. Imam AS anasema:

أَقِیلُوا ذَوِی الْمُرُوءَاتِ عَثَرَاتِهِمْ، فَمَا یَعْثُرُ مِنْهُمْ عَاثِرٌ إِلاَّ وَ یَدُ اللَّهِ بِیَدِهِ یَرْفَعُهُ

Fumbieni macho utelezaji wa watu wenye murua, kwani hatelezi miongoni mwao mwenye kuteleza, ila mkono wa Allah humshika na kumnyanyua.

Muungwana ni mtu ambaye hasiti kufanya jambo lolote jema na zuri kila anapopata fursa hata ndogo ya kufanya hivyo. Popote anapopaswa kufanya uungwana na kutatua matatizo, hasiti hata kidogo kufanya hivyo. Kawaida ya muungwana ni kufanya mambo ya kujitolea na ni mwepesi wa kusamehe. Sasa, wakati inapotokezea mtu muungwana, mtu msafi, mwenye mlahaka mzuri, mwenye tabia njema, mwepesi wa kuwasaidia wengine bila ya majivuno wala masimbulizi, mwenye maadili, wakati inapotokezea mtu wa namna hiyo ameteleza, Imam Ali hapa anawapa nasaha watu kwamba wafumbie macho kuteleza kwake huko, isiwe tena ni kioja na watambue kuwa, kutokana na wema na uungwana wake, Mwenyezi Mungu hamwachi hivi hivi, bali mkono wa Mungu humshika na kumnyanyua. 

Katika hikma hii, Imam Ali (AS) anatilia mkazo mapenzi maalumu aliyo nayo Mwenyezi Mungu kwa watu waungwana, wenye murua na busara. Kwa hata kama kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu hutokezea wakajikwaa, lakini kutokana na usalama wa roho zao na mlahaka wao mzuri na wengine pamoja na uchaji Mungu wao, mara moja Allah huwasaidia na kuwanyanyanyua walipojikwaa na kuwapa taufiki wa kutubu na kurekebisha walipoteleza.  Kwa hiyo, ikiwa watu wa namna hiyo watateleza, wakafanya kosa na kujikwaa, kutokana na pepesi za shertani, kuteleza kwao kunastahiki kufumbiwe macho na kupuuzwa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana zimenukuliwa hadithi kutoka kwa maasumu wakisema kwamba, yeyote anayefichua na kutangaza utelezaji wa watu wa namna hiyo, huwa ametangaza vita na Mwenyezi Mungu. 

Amma kitu ambacho ni kiovu na kimeenea siku hizi kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba wakati mtu mashuhuri na muungwana anapojikwaa na kuteleza kidogo tu, ghafla moja utaona kuteleza kwake huko kunasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kumpaka matope na kumchafulia jina. Inabidi tuwe makini sana kuhusu taarifa zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii. Muuda wote inabidi mtu apime, wakati anapoamua kusambaza kitu chochote, je kitu hicho kina manufaa na je hakina madhara kwa watu wasio na hatia? Baadhi ya wakati utaona kuteleza kidogo tu kunakuzwa kupindukia ili huharibu heshima na utu wa watu. Tunasahau kuwa moja ya sifa za Allah ni ستار العیوب ni Mwingi mno wa kusitiri aibu za waja Wake. Bila ya shaka ni kwa kuzingatia hayo ndio maana katika hikma hii ya 20, Imam Ali AS anatuhimiza tushikamane na maadili na tabia hiyo bora ya kusitiri aibu za wengine.