Hikma za Nahjul Balagha (22)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 22 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 22.
لَنَا حَقٌّ، فَإِنْ أُعْطِینَاهُ، وَ إِلَّا رَکِبْنَا أَعْجَازَ الْإِبِلِ وَ إِنْ طَالَ السُّرَى
“Haki ni yetu, tukipewa, na kama hatukupewa, tutapanda juu ya mgongo wa ngamia na kumuendesha kwa kasi, hata tukitembea mpaka usiku.”
Moja ya mambo ambayo yanaweza kumtokea kila mmoja wetu ni dhulma ambayo kila mmoja wetu anaweza kufanyiwa. Hutokea mara nyingi mtu kuwa dhalimu au kukubali kudhulumiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugumu wa kujihami na kujilinda.
Tab'an Imam Ali AS hawezi kabisa kukubaliana na jambo hilo. Ijapokuwa yeye mwenyewe Imam Ali AS inaonekana kama vile alikubali kudhulumiwa kwa ajili ya kulinda maslahi makubwa zaidi na manufaa muhimu zaidi za jamii ya Kiislamu, lakini hakufanya hivyo kwa kuwa ni mwoga. Ukhalifa wa Waislamu baada ya kifo cha Mtume SAW ilikuwa ni haki yake Imam Ali AS, lakini aliamua kusamehe ili aweze kulinda umoja wa Umma wa Kiislamu. Aliamua kunyamaza na hata alishirikiana na wale waliochukua ukhalifa baada ya kufariki dunia Mtume SAW. Lakini hayo yote hakuyafanya kutokana na kwamba alikuwa dhaifu au mwoga au kuona fakhari kuonewa. Ushahidi wa hayo umo kwenye khutba ya sita ya Nahjul Balagha, ilipotokea fitna ya Jamal na njama ya mapindulizi iliyofanywa na Talha na Zubair. Wakati huo Imam Ali AS alisema: “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu! Nimekuwa nikizuiwa mtawalia kufikia haki yangu, tangu siku alipofariki dunia Mtume SAW na Mwenyezi Mungu alipopokea roho ya mtukufu huyo.
Vile vile katika khutba ya 171 ya Nahjul Balagha tunaona jinsi Imam Ali AS alivyojitetea na kutoa hoja kwa kusema: “Siku moja, mtu mmoja ambaye yeye mwenyewe alikuwa katika mkondo wa wenye uchu wa madaraka asiyeheshimu haki za wengine, aliniambia: Ewe mwana wa Abu Talib, naona una hamu na uchu mkubwa wa ukhalifa. Nilimwambia: “Nyinyi (wapenda ukhalifa) mna pupa zaidi ya kuutia mkononi ukhalifa na mko mbali na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lakini mimi niko karibu naye kimwili na kiroho na pia ninadai haki yangu, na wewe ndiye uliyesimama baina yangu na haki yangu iliyo wazi kabisa na unafanya njama za kuzuia nisipate haki yangu hiyo. Je, anayedai haki yake ndiye mwenye uchu wa mdaraka na mchoyo au yule anayekodolea macho ya tamaa haki za wengine?"
Bila ya shaka yoyote mtu aliye na haki ya kurithi nafasi ya Mtume Mtukufu SAW ni yule ambaye amemkaribia sana Mtume Muhammad SAW katika kila upande na Imam Ali AS ndiye aliyekuwa na sifa hizo. Ndio maana katika hikma hii ya 22 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS amesema: ““Haki ni yetu, tukipewa, na kama hatukupewa, tutapanda juu ya mgongo wa ngamia na kumuendesha kwa kasi, hata tukitembea mpaka usiku.”
Yaani tuna haki ambayo itakuwa vizuri sana kama tutapewa ruhusa ya kuchukua haki yetu lakini tusipopewa tutadumu katika njia ya kupigania haki yetu hata kama tutalazimika kuingia kwenye mashaka na tabu kubwa. Kiujumla ni kwamba, kwa mujibu wa nasaha hizi za Imam AS na ili mtu aweze kupata haki yake, anapaswa kujitahidi kwa njia sahihi na kwa busara kupigania haki yake kwa nguvu zake zote hata kama atalazimika kuvumilia mashaka na matatizo mengi.