Jumamosi, Juni 25, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 19 Ramadhani mwaka 1437 Hijria inayosadifiana na Juni 25 mwaka 2016 Miladia.
Miaka 1397 iliyopita, yaani tarehe 19 Ramadhani mwaka wa 40 Hijria Qamaria, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu wa Mtume Mtukufu SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa anaswali Swala ya alfajiri katika Msikiti wa mji wa Kufa na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na uadilifu. Alipata elimu na maarifa aali ya Kiislamu kutoka kwa Mtume Mtukufu mwenyewe SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu zaidi wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na hata kuhatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu huku akionyesha ushujaa mkubwa katika vita mbalimbali dhidi ya batili. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo, kiasi ambacho moyo wake ulikuwa wenye kuathiriwa sana na kujawa na huruma kwa kuona machozi ya mtoto yatima. Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Imam Ali AS anasema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake.'
XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Msumbiji ilijitangazia uhuru. Ilikuwa mwishoni mwa karne ya 15 wakati kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco Da Gama, lilipowasili nchini Msumbiji na kuanzia wakati huo ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukawa umeanza. Kwa kuzingatia kwamba, katika zama hizo Msumbiji ilikuwa moja kati ya nchi tajiri kwa madini yenye thamani barani Afrika, Wareno walijishughulisha na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Mwaka 1962 harakati ya kupigania uhuru ya Msumbiji FRELIMO, iliongoza mapambano ya silaha dhidi ya mkoloni Mreno. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na siku kama ya leo miaka 194 iliyopita kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Kiafrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kundi hilo la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika wakarejea huko Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.