Aban 13, Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa
Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale mlipo hasa huko nyumbani Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu kuwa, mubukheir wa afya na mnaendelea vyema katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku.
Karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa manasaba wa kumbukumbu ya tarehe 13 Aban inayosadifiana na tarehe 4 Novemba, ambayo inajulikana hapa nchini kama “Siku ya Taifa ya Kupambana na Ustikbari wa Kimataifa na Siku ya Mwanafunzi". Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili mtegee sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.
Katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kama tulivyotangulia kueleza, Aban 13 inajulikana kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa. Tabaan, mnamo tarehe 4 Novemba kulijiri matukio matatu muhimu ingawa ni katika kipindi cha miaka tofauti. Kalenda ya Iran inaonyesha kuwa, mwaka 1964, 1978 na 1979 yalijiri matukio matatu muhimu katika historia ya taifa hili ingawa ni katika tarehe hiyohiyo ya 13 Aban sawa na Novemba 4. Nukta ya pamoja katika matukio matatu hayo ni mapambano ya wananchi wa Iran ya kupigania kujitawala, uhuru na kujitoa kwenye makucha ya satua na ubeberu wa Marekani. Katika tukio la kwanza la mwaka 1964 askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, kuwa taifa huru na kutetea thamani za kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo, kwa sababu utawala wa Shah ulitambua kwamba, kuwepo Imam Khomeini (Rahmatullahi Aleih) nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.
Katika tukio la pili la tarehe 4 Novemba mwaka 1978 kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi."
Na ama katika tukio la tatu lililojiri katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja baada ya Mapinduzi ya Kiislamu wanafunzi na wanachuo wa Tehran walifanya maandamano makubwa katika mji huo kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kubaidishiwa nchini Uturuki Imam Khomeini (MA) na kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa wanafunzi na wanachuo wa Iran. Mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah.
Katika siku hiyo ya tarehe 13 Aban ambayo kama tulivyotangulia kusema ilisadifiana na tarehe 4 Novemba mwaka 1979, katika kulalamikia njama za Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, wanachuo wa Iran walivamia na kuzingira 'Pango la Ujasusi' yaani (Ubalozi wa Marekani) mjini Tehran kwa lengo la kuzuia dola hilo la kibeberu kufikia malengo yake haramu dhidi ya mapinduzi machanga yaliyokuwa yamefikia ushindi Februari mwaka huo. Siku hii inajulikana hapa nchini kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa.
Katika siku hii ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa kinara wao akiwa ni Marekani, hufanyika maandamano kote nchini kuonyesha umoja baina ya kizazi cha zamani na kizazi kipya, ambapo waandamanaji wote hupaza sauti moja kuonyesha kuchukizwa na uistikbari wa kimataifa kwa kupiga nara za 'Mauti kwa Marekani' na 'Mauti kwa Israel'.
Kwa hakika nyaraka zilizofichuliwa katika Pango la Ujasusi zilithibitisha kuwepo uadui na njama kubwa za Marekani dhidi ya taifa la Iran na mfumo wa Kiislamu ambao ulikuwa ungali mchanga.
Njama hizo zinaendelea hadi leo kwa njia mbali mbali na hata baada ya vijana wanamapinduzi na wabunifu kuteka Pango la Ujasusi, lakini adui angali anaendeleza njama zake. Kwa msingi huo kizazi cha vijana wanamapinduzi hii leo kina ufahamu wa kina zaidi kuhusu uadui wa Marekani dhidi ya Iran na hivyo vijana hao walichukua hatua za kuzuia njama zaidi za dola hilo la kibeberu.
Ubunifu wa vijana wa Iran katika kuteka Pango la Ujasusi mjini Tehran ulikuwa na taathira kubwa katika matukio ya Iran kiasi kwamba, Imam Khomeini MA mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliutaja ubunifu na hatua hiyo ya wanafunzi kuwa, 'Mapinduzi ya Pili'.
Kauli hii ya mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitokana na kina cha njama na ukhabithi wa Marekani wakati wa Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na baada ya hapo. Punde baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, dola la kiistikbari la Marekani lilianza kutekeleza njama dhidi ya mapinduzi haya ya watu wa Iran. Lakini kutokana na uangalifu pamoja na mwamko wa watu wa Iran, njama hizo zilisambaratishwa.
Kama alivyosema Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kutekwa Pango la Ujasusi kulikuwa ni jibu muafaka la wananchi dhidi ya uadui wa dola la Marekani lenye uchu wa kuhodhi kila kitu, la kimabavu na la kibeberu, ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likipora utajiri wa Iran lakini mikono yake ikakatwa kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kwa maneno mengine ni kuwa, kutekwa Pango la Ujasusi la Marekani mjini Tehran kulikuwa ni mwisho wa satwa ya dola la kibeberu la Marekni nchini Iran. Jambo hilo linaonyesha wazi kwamba madola makubwa ya kibeberu kama Marekani yatafeli katika njama zao dhidi ya Iran. Kuendelea uadui wa serikali mbali mbali za Marekani dhidi ya Iran kunatokana na kuendelea moyo wa hasira na chuki dhidi ya Marekani walionao wananchi wanamapinduzi wa Iran.
Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba na miongozo yake ya busara kwamba, hatua ya Marekani ya kukiuka ahadi zake na kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA ni misdaki na mfano wa wazi wa kuendelea uadui wake dhidi ya Iran. Aidha Ayatullah Khamenei amekuwa akitilia mkazo nukta ya kwamba, njia muhimu na bora zaidi ya kustawi nchi si katika kufanya mazungumzo au kujikurubisha na Marekani, bali ni kutegemea uwezo wa vijana wa ndani ya nchi na kuwa macho mbele ya sera hasimu za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ukweli wa mambo ni kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulisambaratisha kambi kuu ya Marekani katika kitovu cha Mashariki ya Kati ambalo ni eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta; na Iran ikaja na kaulimbiu ya kupambana na dhulma na ubeberu na kutetea haki za mataifa manyonge jambo ambalo limeifanya kuwa kambi ya kukabiliana na ubeberu wa Marekani duniani.
Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lengo la Wamarekani la kuiwekea mashinikizo ya kila aina Iran ni kujaribu kuwalazimisha wananchi wa Iran waachane na uhuru na heshima yao na waonyeshe kujuta na kuchoshwa na Mapinduzi yao na hivyo kwa mara nyingine waligeuze taifa hili kuwa tegemezi, kibaraka na lililojisalimisha kikamilifu kwa Marekani.
Hapana shaka kuwa, kusimama kidete taifa la Iran, kutokubali kuburuzwa mfumo wa Kiislamu na kuwa macho viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na njama za kila leo za maadui, ndio siri ya kufanikiwa na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Mapinduzi haya yanaingia mwaka wake wa 44 tangu yapate ushindi mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA na licha ya njama za kila upande za maadui zikiongozwa na Marekani, yamepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za kielimu, sayansi, teknolojia na kadhalika na kuwathibitishia walimwengu kwamba, kwa kutegea nguvukazi ya vijana na rasilimali za ndani, taifa lolote linaweza kupiga hatua na kushinda njama za maadui awe ni Marekani au dola jingine lolote lile la kibeberu.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa manasaba wa tarehe 13 Aban sawa na tarehe 4 Novemba ambayo katika kalenda ya Iran inajulikana kama Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.