Jan 01, 2024 04:08 UTC
  • Majina na Lakabu za Bibi Faat'imatu-Zahraa (SalamuLlahi Alayhaa)

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Radio Tehran mpopote pale mlipo wakati huu. Mnamo tarehe 20 Mfunguo Tisa, Jumada-Thani, mwaka wa tano kutokea Kubaathiwa Bwana Mtume, uliosadifiana na mwaka 615 Miladia, nyumba ya Nabii Muhammad (SAW) Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na mkewe Bibi Khadija katika mji wa Makka, iliangazwa na nuru ya kuzaliwa mwana mtukufu. Mwenyezi Mungu aliwabariki watukufu hao wawili binti ambaye, alikuja kuendeleza kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume SAW.

Binti huyo ndiye kielelezo kamili cha Suratul-Kauthar; na Allah SWT akampa majina maalumu, ili awe ruwaza na mfano wa kuigwa na wanadamu wote.

Faatimah ni binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, lakini ana hadhi na adhama, kiasi kwamba ni watu wachache wanaoweza kuifahamu adhama yake hiyo, kama alivyoeleza Imamu Jaafar Sadiq (as) ya kwamba: “Faatimah aliitwa Faatimah, kwa sababu viumbe hawawezi kumfahamu na kumtambua (vilivyo)”.

Kwa sababu hiyo, tunatangulia kukiri na kuungama katika utangulizi huu wa kipindi hiki ya kwamba, tutakayoyasema sisi pia, hayataweza kubainisha wasifu halisi wa Bibi Faatimah (AS). Tutakayoeleza ni yale yaliyopokewa katika aya za Qur’ani na Hadithi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenyewe na kupitia Mtume wake Muhammad SAW na Maimamu (AS) kuhusu Siti huyo mtukufu. Utukufu na daraja ya Faatima (AS) ni ya juu na iliyotukuka, kiasi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ameibainisha kwa maneno bora na mazito alipomwambia Mtume wake:

إِنَّا أَعْطَیْنَاکَ الْکَوْثَرَ ﴿١﴾‏ فَصَلِّ لِرَبِّکَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾‏ إِنَّ شَانِئَکَ هُوَ الْأَبْتَرُ ﴿٣﴾‏

“Hakika Sisi tumekupa wewe Kauthar (kheri na baraka nyingi mno). Basi (kuishukuru at’iya hiyo) Sali kwa ajili ya Mola wako; na unapoanza kwa Takbiiratul-Ihram, ambayo ndiyo mlango wa kuingilia kwenye Sala, jivue kikamilifu na kila kisichokuwa Yeye na ujue kwamba, bila ya shaka adui yako ni abtar, aliyekatikiwa na rehma za Mwenyezi Mungu”.

Naam! Mwenyezi Mungu alimtunukia Nabii wake wa mwisho Kauthar, ambayo ni chemchemi ibubujikayo daima dawamu rehema na fadhila zake Mola; ambayo ni wale tu walio na nyoyo safi na za upendo, ndio wawezao kumiminikiwa na maji angavu ya chemchemi hiyo.

Wasikilizaji wapendwa! Nakupeni mkono wa kukuombeeni kheri na baraka nyinyi nyote ambao mna mapenzi makubwa na kizazi kitoharifu cha Nyumba ya Mtume SAW kwa mnasaba wa mazazi ya mja mteule wa Allah, Bibi Faatimatu-Zahraa (AS)!

Jina, kama mjuavyo wapenzi wasikilizaji, maana yake ni alama na kiitio. Na upaji jina ni namna ya utambulishaji, utafautishaji na upambanuzi wa mtu au kitu. Na sifa, ni mambo yanayowapa umaarufu watu, ambapo kwa kawaida katika majina, zinapatikana pia lakabu. Upaji jina ni utaratibu ulioanzishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni Yeye Mola aliyemwita baba yetu Adam na akampa mama yetu jina la Hawa. Utaratibu wa upaji majina ya mawalii wengi wa Mwenyezi Mungu ulikuwa ni uleule uliokuwepo kwa watu wa jamii zao. Lakini kama inavyobainisha Qur’ani, Mwenyezi Mungu Mtukufu, Yeye Mwenyewe ndiye aliyetoa majina ya baadhi ya mawalii wake, mfano mmojawapo ukiwa ni wa Nabii Isa AS aliposema:

إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِکَةُ یَا مَرْیَمُ إِنَّ اللَّهَ یُبَشِّرُکِ بِکَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِیحُ عِیسَى ابْنُ مَرْیَمَ...

Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu…

Jambo hili, mbali na kuwa ni heshima kwa waja hao, linabainisha pia shakhsia, adhama, ubora na sifa za kipekee walizonazo waja hao wateule. Bibi Faatimah (AS), naye pia ana majina na lakabu kadhaa, ambayo baadhi yao ameyaainisha Mwenyezi Mungu Mwenyewe, na baadhi yao yamebainishwa na waja wateule wa Allah. Imepokelewa katika Hadithi ya kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu, Bibi Faatimah anajulikana kwa majina tisa; ambayo ni: Faat'imah, S'iddiqah, Mubaarakah, T'aahirah, Zakiyyah, Radhiyyah, Mardhiyyah, Muhaddathah na Zahraa.

Jina Faatimah linatokana na neno “fat'ama" lenye maana ya kubanduka na kutenganika. Wakati binti huyo kipenzi cha Bwana Mtume SAW alipozaliwa, Mwenyezi Mungu alimuamuru Malaika akalitamkishe jina Faatimah kwenye ulimi wa Bwana Mtume; naye mtukufu huyo akampa binti yake huyo jina la Faatimah. Faatimah (AS) alipewa jina hilo kwa sababu irada ya Allah ilitaka mtukufu huyo atenganike na awe mbali na kila baya na ovu.

Zahraa, ambalo maana yake ni wema, mwanga na upendo ni lakabu nyingine maarufu zaidi ya Bibi Faatimah (AS). Bwana Mtume SAW amesema, uumbwaji wa Zahraa (SA) umetokana na nuru ya adhama ya Mola Muumba Tabaaraka wa Taalah. Ni nuru hiyohiyo aliyoumbiwa yeye Bwana Mtume SAW na Imamu Ali bin Abi Talib (AS). Ni nuru iliyofichika kwenye hazina ya elimu ya Mwenyezi Mungu. Imam Hassan Askari (as) aliulizwa: Kwa nini Faatimah (AS) aliitwa jina la Zahraa? Imamu akajibu: “kwa sababu mwanzo wa siku uso wake ulikuwa ukimwangazia Amirul Muuminin (AS) mithili ya jua lichomozapo upande wa mashariki; na katikati ya siku ukionekana unaangaza kama mwezi, na wakati jua lilipozama uking’ara kama nyota angavu".

“Siddiqah” maana yake ni kuwa mkweli mno; na ukweli wa Bibi Zahraa haukuishia kwenye maneno yake tu, bali alikuwa mkweli katika matendo yake pia. Alikuwa msema kweli; na akiutekeleza ukweli kwa matendo na hakuikengeuka haki hata chembe. Kupewa Bibi Faatimah na Mwenyezi Mungu lakabu ya Siddiqah kunatokana na umaasumu wa binti huyo wa Mtume wa Allah, kwa sababu kuwa mtu kamili wa haki na kutoteleza katika kuishika haki, katika imani, tabia, maneno na vitendo ni sifa walizonazo waja pekee walio maasumu.

Katika aya ya 75 ya Suratul-Maaidah, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtambulisha mama wa Nabii Isa AS, yaani Bibi Maryam kwa tamko:  وَ أُمُّهُ صِدِّیقَةٌ  yaani na mama yake Isa ni Siddiqah, yenye maana ya aliye mkweli mno. Katika upande mwingine, Bwana Mtume SAW aliwaambia watu:

فاطمة سیدة نساء العالمین من الأوّلین والآخرین

yaani Faatimah, ni mbora wa wanawake wa ulimwengu, kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho (wao). Kwa hiyo wakati Qur'ani Tukufu inapothibitisha kwamba Bibi Maryam AS ni maasumu na mkweli mno, yaani Siddiqah; Bibi Faatimah (SA), ambaye ni Siddiqatul-Kubra aliye na ubora na daraja ya juu zaidi ya utukufu kuliko wa Bibi Maryam, atakuwa na umaasumu wa kiwango cha juu zaidi.

Jina la Muhaddathah huitwa mtu anayesemezwa na Malaika. Qur'ani Tukufu imesimulia mara kadhaa Malaika kuzungumza na watu wasio Mitume. Wakati Bibi Maryam alipokuwa na mimba ya Nabii Isa (as), yalitokea mazungumzo baina yake na Malaika ambayo yametajwa katika aya ya 18 hadi 21 za Suratu-Maryam. Katika Hadithi, Bibi Faatimah (as) ametajwa sana kwa jina hilo. Kwa mujibu wa Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imamu Jaafar Sadiq (as), baada ya kuaga dunia Bwana Mtume SAW, Bibi Faatimah aliishi kwa siku zingine 75 tu; na kutokana na kuwa na huzuni na majonzi makubwa ya kuondokewa na baba yake, Malaika Jibril alikuwa akimjia kumfariji na kumliwaza na kumpa habari kuhusu baba yake, hali tukufu aliyonayo huko aliko na vilevile yatakayokuja kutokezea kwa kizazi chake baada ya kuondoka Bwana Mtume SAW. Hayo yote yalikuwa yakiandikwa na Imamu Ali (AS) na ndio hiyo ijulikanayo kama Mas-hafu ya Faatimah.

Majina mengine ya Bibi Faatimah ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtambua kwayo mja wake huyo mteule ni Raadhiyah na Mardhiyyah. Maana ya Raadhiyah ni mtu aliye radhi na aliyeridhia; na maana ya Mardhiyyah ni mtu aliyeridhiwa na aliyepata radhi. Katika aya za mwishoni mwa Suratul-Bayyinah, Mwenyezi Mungu anatubainishia siri ya majina haya aliposema:

إِنَّ الَّذِینَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِکَ هُمْ خَیْرُ الْبَرِیَّةِ

Hakika walio amini na wakatenda mema, hao ndio wabora wa viumbe.

 Kisha akayataja malipo ya wabora hao wa viumbe aliposema:

جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِی مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِینَ فِیهَا أَبَدًا ۖ رَّضِیَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ ذَٰلِکَ لِمَنْ خَشِیَ رَبَّهُ ﴿٨﴾‏

Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi.

Bibi Faatimah (SA), ni mmoja wa waja bora wa Mwenyezi Mungu, yaani Khairul-Bariyyah ambaye amefikia daraja ya kuridhiwa na Mola, naye pia akawa radhi na Mola wake. Maneno: ذَٰلِکَ لِمَنْ خَشِیَ رَبَّهُ  hayo ni malipo kwa aliyemhofu Mola wake Mlezi yanaonyesha kuwa, baraka zote hizo zinatokana na "khofu juu ya Allah". Na ni khofu hiyo inayotokana na kuitambua haiba ya Mola ndiyo inayomfanya mja huyo mteule awe mtiifu na mwenye taqwa na mfanyaji amali njema. Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wameiambatisha aya hii ya mwisho ya Suratul-Bayyinah na sehemu ya aya ya 28 ya Suratu-Faat'ir isemayo:

إِنَّمَا یَخْشَى اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ

Kwa hakika wanao mkhofu Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni, na kufikia hitimisho kwamba, khofu hiyo ni matunda ya kuwa na ufahamu na utambuzi wa batini wa kumjua Mwenyezi Mungu; na Faatimah (as) alifikia kilele cha utambuzi huo. Kwa maelezo haya, huenda ndipo tutapoweza kuyafahamu vizuri zaidi maneno ya Mtume wa Allah alipomhutubu binti yake ya kwamba: یَا فَاطِمَةُ إِنَّ اَللَّهَ تَبَارَکَ وَ تَعَالَى لَیَغْضَبُ لِغَضَبِکِ وَ یَرْضَى لِرِضَاکِ  kwamba ewe Faatimah, hakika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anaghadhibika kwa kughadhibika kwako na anaridhika kwa kuridhika kwako".

Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye maneno yake, -kwa kusadikishwa na Qur'ani Tukufu- ni maneno ya wahyi na katu hasemi kitu chochote kwa hawaa na matamanio ya nafsi yake, na ambaye anapofanya jambo, anapokuwa ametulia, anaposema kitu na anaponyamaza kimya, bali hata kufurahi na kughadhibika kwake katika hali ya umaasumu kunaendana na kufurahi na kudhaghibika Allah SWT, amenena yafuatayo kumhusu binti yake Faatimah (AS): "Faatimah ni sehemu itokanayo na mimi, yeyote amfurahishaye yeye amenifurahisha mimi, na yeyote amghadhibishaye yeye, basi amenighadhibisha mimi". Tusisahau kwamba, kama mtu hatokuwa ametakasika na hawaa na matamanio ya nafsi, kuridhika na kughadhibika kwake hakutakuwa kipimo cha kupambanulia haki na batili. Lakini kama atakuwa mwanadamu mwenye ukamilifu wa kiutu, aliyetakasika na uchafu wa hawaa na matamanio ya nafsi, kuridhika kwake na kughadhibika kwake kwa namna yoyote iwayo, kutakuwa kipimo cha kupambanua na kubaini haki na batili.

Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyingine tena nachukua fursa hii kukupeni mkono wa kukuombeeni kheri na baraka kwa mnasaba huu adhimu wa mazazi ya Bibi Faatimah (AS) na tunakamilisha kipindi chetu hiki kwa kumsalia na kumtakia rehma na amani mtukufu huyo kwa kumuomba Allah kwa kusema: "Ewe Mola, mshushie rehma na amani Faatimah, pamoja na baba yake mtukufu, na mume wake muadhamu pamoja na watoto wake watoharifu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

 

 

Tags