Feb 11, 2024 04:27 UTC
  • Mapinduzi ya Kiisamu; chimbuko la mageuzi ya kiroho na kimaanawi ya wananchi wa Iran

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi maalumu vinavyokujieni kwa mnasaba wa Alfajiri Kumi kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya Iran yaliyotokea 1979

 

Kipindi chetu cha leo kitazungumziia jinsi mapinduzi haya ya Kiislamu yalivyokuwa na mchango mkubwa katika kuleta mageuzi na mabadiliko ya kiroho na kimaanawi kwa wananchi wa Iran. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

 

Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotokea nchini Iran mnamo Februari 1979 (22 1357 Bahman) yalileta mabadiliko muhimu ambayo yaliathiri sio Iran tu, bali hata nchi zingine pia. Tofauti muhimu zaidi inayoitofautisha ya harakati hii ya kipekee na mapinduzi mengine yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya dunia ni kwamba, mapinduzi haya yalikuwa ni ya Kiislamu na kidini. Bila shaka Imam Khomeini (RA), kiongozi mkubwa na mwanamageuzi shupavu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akiwa mwanazuoni wa ngazi za juu wa kidini na mlinganiaji wa mafundisho ya Kiislamu, alikuwa na mchango mkubwa katika mwelekeo wa kidini na kiroho wa mapinduzi hayo.

Imam Khomeini alikuwa na ushawishi na umaarufu mkubwa miongoni mwa watu wa Iran kiasi kwamba, walikuwa wakiikubali miongozo yake kwa moyo wote na kuifanyia kazi pasi na kusita. Huba na mapenzi haya ya wananchi wa Iran pamoja na utii na uaminifu wao kwake ulidhihirishwa zaidi katika mapokezi makubwa na yasiyoweza kusahaulika ya Imam Khomeini na wananchi pale alipowasili Iran tarehe 12 Bahman 1357 Hijria Shamsia (tarehe 1 Februari 1979) akitokea uhamishoni nchini Ufaransa, na hali hiyo iliendelea hadi mwishoni mwa umri wa shakhsia huyo mkubwa.

Imamu Khomeini alipowasili Tehran kutoka uhamishoni Ufaransa na jinsi alivyokewa na mamilioni ya watu

 

Wakati kiongozi huyu mwenye busara na mtu wa watu alipotaja maadili ya Kiislamu kuwa msingi wa mapinduzi, watu wa Iran, ambao kimsingi walikuwa wanajua mafundisho haya yenye nuru na yaliyojaa maanawi na walikuwa na ufahamu kuhusu historia ya ustaarabu mzuri wa Kiislamu katika historia yao, haraka walikubali na kuitikia mwito wake bila ya kusita. Kwa muktadha huo, baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, moyo wa mafundisho ya Uislamu ya kumjenga mwanadamu ulitawala anga ya jamii ya Iran kwa ajili ya kuandaa uwanja na mazingira ya ukuaji na ukamilifu wa kimaanawi na kimaadili wa watu wa Iran.

 

Waislamu wa Iran walitaka kuwepo kwa jamii na mfumo wa kisiasa unaojikita  katika maadili ya kidini na kiroho, katika hali ambayo katika nchi za Magharibi; kwa kuenea kwa propaganda za vyombo vya habari, kutoamini Mungu, uchafu wa kingono na kuzorota kwa maadili kulikuwa kumeshika kasi.

Lakini Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa ni harakati ya Kimungu na kidini dhidi ya mkondo huu wa batili ambao unakinzana na fitra na maumbile ya mwanadamu, na kwa sababu hiyo, yalichochea hasira za serikali za magharibi. Baada ya mapinduzi hayo, mwelekeo wa watu wa Iran, hususan vijana, katika mila na desturi za kidini na maadili uliongezeka.

Kimsingi ni kuwa, baada ya miaka mingi ya propaganda za kupinga dini za utawala wa kifalme wa Pahlavi, taifa la Iran lilipata tena utambulisho wake wa kidini. Kwa upande mwingine, imani ya watu juu ya maadili halisi ya Kiislamu iliongezeka kwa miongozo ya Imam Khomeini na viongozi wengine wa kidini, uchapishaji wa vitabu vya kidini na shughuli za kisanii za kidini, ni mambo ambayo yakawa yakitekelezwa kwa wigo mpana zaidi; na wananchi wa Iran wakawa wakitekeleza mafundisho ya Uislamu kwa ufahamu na usahihi zaidi.

Katika mazingira haya, misikiti ilichukua nafasi muhimu katika kudhihirisha na kuonyesha maadili na thamani za Kiislamu katika mapinduzi ya Iran.

Waumini wakiwa katika ibada ya itikafu

Wakati wa kujiri harakati za mapinduzi, maeneo haya matakatifu yalikuwa ni kitovu cha kukusanya wanamapinduzi na kubadilishana taarifa na kupanga mbinu na mikakati ya kuendesha mapambano dhidi ya utawala wa Pahlavi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi yay Kiislamu, misikiti hiyo ilipata nguvu mpya kwa wingi wa mahudhurio ya watu na kuendeleza ibada mbalimbali za kidini, zikiwemo Sala za jamaa, kusoma Quran, dua na kutekeleza shughuli mbalimbali za minasaba wa kidini. Aidha, vijana wenye hamasa na wa Kimapinduzi wa Iran waliigeuza misikiti kuwa ngome na vituo vya kufanya kazi za kitamaduni na kuwasaidia wasiojiweza.

Wakati jeshi la Saddam dikteta wa zamani wa Iraq lilipoishambulia Iran mwaka 1980, misikiti ilichukua jukumu la kuandaa wapiganaji na kuwapeleka kwenye medani ya vita, pamoja na kukusanya na kupeleka misaada ya watu kwa wanamapambano hao. Kwa upande mwingine, hatua kwa hatua baadhi ya kazi na utendaji wa msikiti ukazidi kudhihirika na mahudhurio ya watu ndani ya misikiti yakawa na wigo mpana zaidi ambapo moja ya hayo na muhimu zaidi ni ibada ya itikafu.

Katika marasimu haya ya ya kiroho, waumini hukusanyika na kubaklia msikitini kwa muda wa siku tatu ambapo hufunga Saumu, huomba dua na kunong'ona na Mwenyezi Muungu na kuanzisha uhusiano wa karibu wa kiroho na Mola wao Muumba.

Hata hivyo, kilele cha mielekeo ya kiroho, hasa miongoni mwa vijana, kilidhihirika wakati wa kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu mkabala wa mashambulio ya jeshi la Saddam kiongozi wa zamani wa Iraq kuanzia 1980 hadi 1988.

Mmoja ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yay Iran katika medani ya Azadi 

 

Katika medani za vita, wapiganaji wa Kiislamu walikuwa wakipigana kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwa kutawasali kwa Mtume na familia yake (SAW) na kutamani kuuawa shahidi. Moyo na ari hii ya kimaanawi ilikuwa ni matokeo ya ibada yao, ikhlasi na kujijenga kwao kiroho na hivyo kuwageuza kuwa Mujahidina wachamungu, wajasiri na wanaotafuta na kupigania haki.

Dhihirisho jengine la kupanuka kwa hali ya kiroho baada ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni kuwepo kwa watu wengi katika haram takatifu za Maimamu (a.s.) na watoto wao watukufu kwa ajili ya kufanya ibada na kupata hali ya kiroho na kueleza haja zao. Vilevile kila mwaka husherehekea uzawa na maombolezo ya kuuawa shahidi familia ya Mtume (SAW).  

Moja ya dhihirisho kubwa la kuonyesha huba na mapenzi kwa viongozi hao wa kidini, ni ushiriki wa mamilioni ya Wairani katika matembezi makubwa na ya hamasa ya Arubaini huko Iraq, ambayo hufanyika kumuomboleza Imam Hussein (a.s.). Kwa maelezo hayo, inaweza kusemwa kwamba, wananchi wa Kiislamu wa Iran wamepata ufahamu mpya na wa kina wa dini yao kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na uwanja wa kupata maisha ya kiroho na maadili umeandaliwa kikamilifu.

 

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki, tukutane tena siku nyingine na katika kipindi kipindi kingine maalumu cha kuelekea kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuuh.

Tags