Oct 07, 2023 15:14 UTC
  • Haniya: Kimbunga cha Al-Aqsa kimeanzia Gaza na kitafika hadi Ufukwe wa Magharibi

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: Kimbunga cha Al-Aqsa kimeanzia Gaza na kitafika hadi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, nje yake na popote pale walipo wananchi wa Palestina.

Leo asubuhi, vikosi vya Muqawama vya Palestina vimeshambulia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ikiwemo Tel Aviv na Ashdod kwa makombora na maroketi zaidi ya 7,000 katika operesheni iliyopewa jina la "Kimbunga cha Al-Aqsa".
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sama, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema, sababu kuu ya Muqawama kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni hujuma za mtawalia zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Msikiti wa  Al-Aqsa, matakatifu na mateka wa Kipalestina.
Haniya amebainisha kuwa, katika siku za hivi karibuni, maelfu ya walowezi watenda jinai na mafashisti wamevamia na kuvunjia heshima mahala aliposimama Bwana Mtume SAW na kufanya sherehe zao za kidini, na kwamba hatua hiyo ni utangulizi wa Wazayuni kulidhibiti eneo hilo takatifu.
 
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas amedokeza kuwa Umma wote wa Kiislamu kuanzia mashariki hadi magharibi na kutoka kaskazini hadi kusini utaulinda Msikiti wa Al-Aqsa, na akawataka Waislamu wote na watetezi wa uhuru kote duniani kushiriki katika vita hivyo vya haki na uadilifu kwa ajili ya kupahami mahali hapo patakatifu.
Askari wa Kizayuni aliyeangamizwa katika Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa

Ismail Haniya amesisitiza kuwa, ili kuizingira Gaza, adui Mzayuni anauvamia na kuushambulia Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kujenga vitongoji vya walowezi ili awahamishe wananchi wa Palestina katika ardhi yao.

 
Kufuatia jinai za mtawalia zinazofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na maeneo matakatifu ya Waislamu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, leo wanamapambano wa Muqawama wamenzisha operesheni kabambe za mashambulio ya pande zote dhidi ya Wazayuni maghasibu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kutokea angani, nchi kavu na baharini.
 
Kwa kutumia maparachuti, makomandoo kadhaa wa muqawama wametua katika baadhi ya maeneo ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kupambana na adui mzayuni.
 
Katika operesheni hizo kabambe za muqawama wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na kwa mujibu wa ripoti tulizopokea hadi sasa wazayuni wasiopungua 100 wameangamizwa na mamia ya wengine wamejeruhiwa.
Wakati huohuo harakati ya Hamas imetangaza kuwa, imekamata mateka idadi kubwa ya askari wa Kizayuni katika operesheni ya Kimbunga cha Aqsa.
Sambamba na hayo ripoti za hivi punde kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu zinaeleza kuwa, Wapalestina wapatao 200 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 1,600 wamejeruhiwa katika mashambulio ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa.../

 

Tags