May 04, 2024 09:54 UTC
  • Algeria yataka kikao cha Baraza la Usalama kujadili makaburi ya halaiki Gaza

Serikali ya Algeria imetoa mwito wa kufanyika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadili suala la makaburi ya halaiki huko Gaza Palestina.

Algeria, ikiwa mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama, imetaka kufanyika kwa kikao hicho kwa faragha Jumanne ijayo.

Kabla ya hapo Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa alitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu makaburi ya umati yaliyogunduliwa katika hospitali kuu mbili za Ukanda wa Gaza.

Wito huo wa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa unafuatia ule uliotolewa Stefan Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye ametaka kufanyike uchunguzi wa kuaminika, kamili na huru kuhusu makaburi ya halaiki yaliyogunduliwa katika Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya wamajeshi wa Israel kuondoka katika eneo hilo.

Ukumbi wa mikutano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Afrika Kusini nayo tayari imetoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu makaburi ya umati yaliyogunduliwa katika Ukanda wa Gaza.

Miito hiyo inatolewa baada ya hivi karibunii wafanyakazi wa utumishi wa umma huko Gaza kuopoa miili ya Wapalestina 283 katika makaburi kadhaa ya umati katika yadi ya Hospitali ya Nasser, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Baadhi ya waliouawa walikuwa wamefungwa macho na kufungwa pingu.