May 22, 2024 10:41 UTC
  • Ujumbe wa rambirambi wa serikali na taifa la Iraq kwa Kiongozi Muadhamu na taifa la Iran

Kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na wenzake katika ajali ya helikopta, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani, amefika Tehran na kukutana na Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kumpa salamu za rambirambi  kwa niaba ya serikali na taifa la Iraq.

Kwa mujibu wa shirika la habari IRIB, katika mazungumzo na Kiongozi wa Mapinduzi, Al Sudani amemfahamisha kuwa: ''Katika mazingira haya ya majonzi, nimekuja kukutana nawe ili kueleza masikitiko, huzuni na rambirambi za serikali na taifa la Iraq kwa serikali na taifa la Iran. Tuliyoyaona kutoka kwa Bwana Raisi, rais aliyeuawa shahidi wa Iran, hayakuwa ila uaminifu, unyoofu, usafi, kazi na juhudi na huduma kwa wananchi."

Waziri Mkuu wa Iraq ameashiria pia mahudhurio ya mamilioni ya wananchi katika hafla ya mazishi ya rais aliyekufa shahidi wa Iran na kusema: "Picha nilizoziona kwenye televisheni leo zimekuwa na ujumbe wa wazi, ujumbe muhimu zaidi ambao ni kina cha taswira zenye nguvu zinazoashiria uhusiano kati ya wananchi na viongozi katika Jamhuri ya Kiislamu, licha ya kuwepo mashinikizo na vikwazo vyote na tukio hili ni la kusikitisha."

Al Sudani ameendelea kusema: "Ujumbe mwingine wa kushiriki mamilioni ya watu katika hafla ya mazishi ni kwamba tuwahudumia wananchi na mazishi haya adhimu ni matokeo ya kuwahudumia watu na somo hili linapaswa kuwa somo letu pia huko Iraq."

Msafara wa Mashahidi

Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei amemshukuru Waziri Mkuu wa Iraq kwa safari yake mjini Tehran kwa ajili ya kutoa salamu za rambirambi na kusema: "Tumepoteza shakhsia adhimu. Mheshimiwa Rais alikuwa ni ndugu mzuri sana na afisa mahiri, mwenye uwezo, mkweli na makini."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Hivi sasa Bwana Mokhber amebeba jukumu zito kwa mujibu wa katiba, na Mwenyezi Mungu akipenda, njia hiyo hiyo ya ushirikiano na makubaliano na serikali ya Iraq itaendelea."