May 22, 2024 08:30 UTC
  • Uwezo wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kikabiliana na matukio yasiyotabirika

Kuanza kazi kwa awamu ya 6 ya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuainishwa tarehe 28 June kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mpya wa Rais nchini kunaonyesha wazi uwezo mkubwa wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na matukio yanayojitokeza katika nyakati tofauti.

Jumatatu tarehe 20 Mei kulitangazwa habari ya kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na ujumbe wa ngazi za juu alioandamana nao katika ajali ya helikopta. Siku moja baada ya tukio hili chungu na la kusikitisha, kikao cha sita cha Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kilitakikana kufunguliwa.

Seyyed Ebrahim Raisi alikuwa mmoja wa wajumbe wa mkutano huo na mmoja wa watu waliokuwa na nafasi nzuri ya kuchukua nafasi ya mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa baraza hilo. Wakati wananchi wa Iran wakimuomboleza rais wao aliyekufa shahidi, kikao cha sita cha baraza hilo kilifanyika Jumanne kama ilivyotarajiwa na bila ya tatizo lolote.

Uchaguzi wa awamu ya sita ya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ulifanyika Ijumaa Machi 1, mwaka huu sambamba na uchaguzi wa awamu ya kumi na mbili wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge. Muda wa uwakilishi wa wajumbe wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ni wa miaka 8 ambapo lina wajumbe wapatao 88. Mohammad Ali Mowahedi Kermani, amechaguliwa kuwa mkuu wa baraza hilo kwa kura 55. Kwa mujibu wa sheria za ndani za baraza hilo la Wataalamu, Muwahedi Kermani ataliongoza baraza hilo kwa kwa muda wa miaka miwili.

Kufanyika kwa hafla ya ufunguzi wa awamu ya 6 ya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu katika tarehe iliyotangazwa huko nyuma na bila kucheleweshwa hata kwa siku moja kutokana na kuuawa shahidi Rais Ebrahim Raisi, Seyyed Mohammad Ali Aal Hashem, mwakilishi wa watu wa Azerbaijan Mashariki katika baraza hilo pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu serikalini, kunaonyesha kwamba matukio muhimu ya kisiasa nchini Iran hayaathiriwi na matukio yasiyotarajiwa na wala hayaathiri kwa vyo vyote vile uendeshaji wa nchi.

Mazishi ya Rais Raisi na wenzake mjini Tehran

Wakati huo huo, katika siku ambayo rais aliuawa shahidi, kwa upande mmoja, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alimuidhinisha makamu wa kwanza wa rais kusimamia shughuli za serikali na kuamuru uchaguzi mpya wa rais ufanyike ndani ya miaka 50 kama inavyosema katiba ya nchi. Kwa upande mwingine, Wizara ya Mambo ya Ndani pia imependekeza kwa Baraza la Wataalamu, tarehe ya kufanyika uchaguzi, tarehe ambayo tayari imekubaliwa na baraza hilo.

Ibara ya 131 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema: "Ikitokea kifo, kufukuzwa, kujiuzulu, kutokuwepo au kuugua rais kwa zaidi ya miezi miwili, au ikitokea kwamba muda wa urais umeisha na rais mpya bado hajachaguliwa kutokana na vikwazo au mambo mengine kama hayo, makamu wa kwanza wa rais atachukua nafasi na kutekeleza majukumu yake kwa idhini ya Kiongozi Muadhamu, ambapo baraza litakaloundwa na spika wa bunge, mkuu wa vyombo vya mahakama makamu wa kwanza wa rais litaandaa mazingira ya kuchaguliwa rais mpya ndani ya muda usiozidi siku 50. Iwapo makamu wa rais atafariki au kuibuka masuala mengine yanayomzuia kutekeleza majukumu yake, au rais kutokuwa na makamu wake wa kwanza, Kiongozi Muadhamu atamteua mtu mwingine kuchukua mahala pake."

Kuanza mchakato wa kumchagua rais mpya bila shaka ni kielelezo cha uwezo mkubwa wa kisheria ilionao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na hali ngumu bila ya kusababisha matatizo katika uendeshaji wa nchi. Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema siku ya Jumapili: "Watu wetu wapendwa wanapaswa kuwa na yakini kwamba hakutakuwa na tatizo lolote katika uendeshaji wa nchi." Imani hii thabiti ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi pia inatokana na uwezo huo mkubwa wa kisheria uliopo nchini.

Tags