May 22, 2024 10:36 UTC
  • Kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri Iran chaongozwa na kaimu Rais Mohammad Mokhber

Kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri la serikali ya Iran baada ya kufa shahidi Sayyid Ebrahim Raisi kimefanyika chini ya uenyekiti wa kaimu rais Mohammad Mokhbar na kuwashirikisha wanabaraza wote.

Katika kikao hicho, Mohammad Mokhber amesema kifo cha kishahidi cha Ayatullah Raisi kilikuwa na jumbe mbili maalum. Amefafanua kwa kusema: "Mapokezi ya kiwiliwili cha shahid Raisi na mashahidi wengine huko Tabriz, Qom na Tehran yamethibitisha kwamba itikadi kuhusu Imam Khomeini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zimekita mizizi katika maisha ya watu wa Iran na hazitayumbishwa na tukio lolote.

Kaimu Rais amemtaja Shahid Raisi kuwa aliyefungamana na itikadi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: 'Tukio la hivi karibuni llimepelekea wananchi washikamane zaidi na mafundisho na malengo makubwa ya mfumo wa Kiislamu

Mokhber amesema kuhudhuria mamilioni katika shughuli za kuwaaga mashahidi ni ishara ya utambuzi wa kina wa kuhudumu katika njia ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa: 'Shahidi Ayatullah Raisi kwa mara nyingine tena ametuthibitishia sisi sote kwamba tendo jema kubwa zaidi ni kuwatumikia wananchi kwa uaminifu kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kwamba tukifuata njia hii, tutakuwa na mwisho mwema.'

Msafara wa kuwaaga mashahidi

Kaimu Rais wa Iran, katika kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, amewataka tena wajumbe wote kuendeleza sera ya Marehemu Rais bila kuchelewa na kwa moyo ule ule wa siku zote, na kuwaonyesha wananchi katika kipindi hiki kilichobakia cha serikali kuwa matokeo ya jitihada za serikali ya Shahidi Raisi yatazaa matunda katika mustakabali wa Iran.

Mokhber pia amegusia mipango iliyofanywa kwa ajili ya uchaguzi ujao wa rais na kuwataka wote katika baraza la mawaziri kufanya juhudi maradufu  ili kudumisha maelewano ya kitaifa na kuongeza kuridhika na ushiriki wa wananchi.