Jun 23, 2024 02:47 UTC
  • Vyombo vya habari vya Marekani: Israel imeachana na nia ya kuimaliza HAMAS baada ya kushindwa

Shirika la habari la Bloomberg limefichua katika ripoti yake kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni limeachana na lengo lake kuu lililotajwa katika shambulio la Gaza ambalo ni kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Shirika hilo la habari la Marekani limemnukuu Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel akikiri waziwazi kuwa, madai ya wanasiasa wa utawala wa Kizayuni ya kuwa lengo lao ni kuiangamiza HAMAS ni kujaribu kuwapumbaza Waisraeli."

Kwa mara nyingine tena msemaji huyo wa jeshi la Israel amesema: "Hamas ni fikra, Hamas ni taasisi. Hamas imekita mizizi katika mioyo ya watu -- yeyote anayefikiri tunaweza kuisambaratisha Hamas anakosea." .

Shirika hilo la habari la Bloomberg la Marekani limesema katika uchambuzi wake kwamba, ukiachana na kukiri huko jeshi lenyewe la Israel, lakini pia uhakika utabakia kuwa ni ule ule kwamba Hamas haijatoweka, ina maelfu ya askari na mtandao mkubwa wa mahandaki kwenye Ukanda wa Ghaza. 

Wanamapambano wa HAMAS

 

Shirika hilo la habari la Marekani pia limesema kwamba, hali hiyo imemuweka kwenye wakati mgumu sana waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu na hana namna yoyote ya kutangaza ushindi katika vita hivyo wala kudai kuwa amefanikisha malengo aliyotangaza kabla ya vita hivyo ikiwemo kuingamiza Hamas na kukomboa mateka wa Kizayuni.

Wanajeshi makatili wa Israel wamekuwa wakifanya mauaji ya kutisha kwenye Ukanda wa Ghaza kwa zaidi ya miezi minane sasa, na kusababisha janga kubwa la kibinadamu mbali na uharibifu mkubwa na kuua zaidi ya watu 37,300 hasa raia wa kawaida, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo.