Jun 22, 2024 10:32 UTC
  • Guterres: Dunia haiwezi kustahamili Lebanon iwe Gaza nyingine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasi wasi mkubwa alionao kutokana na kushtadi taharuki baina ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Israel na kusisitiza kuwa, dunia haiwezi kuvumilia Lebanon igeuzwe Gaza nyingine.

Antonio Guterres ametoa indhari hiyo katika kikao na waandishi wa habari mjini New York, wakati huu ambapo vita vya maneno na mashambulizi yanatokota baina ya Hizbullah na Israel.

Guterres ameeleza bayana kuwa, "Pande husika zinapasa kutangaza upya haraka iwezekanavyo utekelezaji kamili wa Azimio Nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na zirejee katika hali ya kutokuwa na uhasama baina yao."

Katibu Mkuu wa UN amesema: Watoto wanapaswa kulindwa. Watoto, waandishi wa habari na wahudumu wa afya hawapaswi kulengwa; na wakimbizi wa ndani wanastahili kuruhusiwa kurejea kwenye makazi yao.

Onyo hili la Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa limekuja huku Harakati ya Hizbullah ikisisitiza kuwa ina uwezo wa kujilinda yenyewe na kuihami Lebanon.

Mashambulizi ya makomobora ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya Wazayuni

Jumatano iliyopita, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah, aliapa kwamba "hakuna sehemu" katika maeneo yanayokaliwa na Israel itakayosalimika na makombora yetu ikiwa vita vikubwa vitaanza.

Katika hatua nyingine, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon jana Ijumaa, kwa mara nyingne tena ilishambulia kwa maroketi na ndege zisizo na rubani maeneo na kambi kadhaa za kijeshi za utawala wa Kizayuni Israel huko kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kujibu chokochoko za jeshi hilo katili. 

Inaelezwa kuwa, Hizbullah imeshambulia kambi ya kijeshi ya Wazayuni ya Ras Naqoura kwa kutumia droni za kamikaze, kujibu hujuma za kinyama za Israel dhidi ya kijiji cha Deir Kifa cha kusini mwa Lebanon. Wanajihadi wa Hizbullah pia wameshambulia maeneo ya Ruwaisat al-Qarn na Zibdin yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia maroketi.

 

Tags