Israel, utawala mbovu zaidi wa kuwekeza, hasara wanayopata Wazayuni haivumiliki
(last modified Sat, 22 Jun 2024 02:25:14 GMT )
Jun 22, 2024 02:25 UTC
  • Israel, utawala mbovu zaidi wa kuwekeza, hasara wanayopata Wazayuni haivumiliki

Vita vinavyoendelea huko Ghaza na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina zinaendelea kuusababishia hasara kubwa pia utawala wa Kizayuni hasa za kijeshi na kiuchumi.

Wimbi la walowezi wa Kizayuni wanaokimbia ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, limeongezeka mno tangu vilipoanza vita vya Ghaza kwa namna ambayo hali hiyo haijawahi kushuhudiwa mfano wake katika kipindi chote cha historia iliyojaa laana ya Israel. Tafiti zinazofanywa mara kwa mara na duru zanyewe za kizayuni  zinaonesha kuwa mwaka jana 2023 idadi ya wawekezaji wanaoondoa mitaji yao na kusimamisha miradi yao huko Israel imeongezeka kwa asilimia 232.

Israel, ambayo inajaribu kuhalalisha jinai zake kwa muda mrefu sasa na hususan wakati huu wa vita vyake vya kikatili dhidi ya Ghaza, hivi sasa imefedheheka vibaya mno hata kwa raia wa nchi za Magharibi.

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Hii ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa, Israel imeondolewa kwenye orodha ya maeneo 10 bora ambayo mamilionea duniani wanapendelea kuwekeza miradi yao. Tovuti ya Marekani ya "Business Insider" imesema katika ripoti yake kuwa, mwaka 2023, wimbi la kuhama wawekezaji kutoka maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni liliongezeka kwa asilimia 232. 

Tangu Israel ilipoanzisha vita vipya dhidi ya Ghaza mwezi Oktoba 2023 hadi hivi sasa imeshaua shahidi karibu Wapalestina 38,000 na makukmi ya maelfu ya wengine wameshajeruhiwa. Hivi sasa wakaazi wa Ghaza wanateseka kwa uhaba mkubwa wa chakula, maji, dawa na mafuta, na maisha ya watoto na wazee katika ukanda huo yako hatarini zaidi kuliko wakati wowote nyuma.